DODOMA-Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)anayeshughulikia Huduma za Lishe, Bw. Luitfrid Nnally amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la hamasa kwa wananchi katika kutekeleza afua muhimu za lishe.
Ni tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Lishe na kupelekea kupungua kwa matatizo yatokanayo na upungufu wa lishe bora kwa kiasi kikubwa.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa Nane wa Tathimini ya Mkataba wa Lishe na Kutambulisha Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika Afya ya Mama na Mtoto (TMCHIP) uliofanyika katika Ukumbi wa Jiji Mtumba jijini Dodoma.
Mkataba huo wa lishe ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais alimwagiza Mheshimiwa Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI asaini Mkataba na Wakuu wote wa mikoa ili kuimarisha usimamizi katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lengo ni kupunguza changamoto ya lishe na athari zake.
Bw. Nnally amesisitiza kuwa matatizo mbalimbali ya lishe ni miongoni mwa changamoto zinazopunguza kasi ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo katika Taifa letu.
Hivyo, jitihada kubwa zinahitajika ili kuyatatua ikiwa ni pamoja na kutoa elimu, kwani huduma za lishe zinalenga kuimarisha rasilimali watu ambao ni mtaji wa kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na maradhi, umasikini na ujinga na hivyo kuongeza uwezo wa Kukuza Uchumi katika Taifa.
Mkutano huo ambao mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mhe. Mohamed Mchengerwa umehudhuriwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga wa Kuu wa Mikoa na wa Wa halmashauri na Maafisa lishe wa Mikoa.