MOROGORO-Wauguzi 49 wamehitimu mafunzo ya Diploma ya Uuguzi Ukunga katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Morogoro kupitia Mradi wa Mkapa Fellow Scholarship, unaotekelezwa na Mkapa Foundation kwa ufadhili wa Benki ya NBC.
Mafunzo haya yalitolewa ili kuboresha ujuzi na maarifa kwa wauguzi walio kwenye ajira (in-service) katika kukabiliana na changamoto za uzazi kwenye vituo vya huduma za afya wanavyofanyia kazi.
Morogoro ni miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa idadi kubwa ya vifo vya mama na mtoto Tanzania na kupelekea kuchagulia kwa awamu ya kwanza ya mradi huu, ambao utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kwa kuboresha uwezo wa kitaalamu wa wauguzi.
Mkapa Foundation imeendelea kuwa mdau muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini kupitia eneo la rasilimali watu katika sekta ya afya. Kupitia mradi huu na kwa ufadhili wa benki ya NBC,hadi ifikapo mwaka 2028 takribani wauguzi wakunga 500 watanufaika na ufadhili huu wa masomo.