Wasalitiana katika maandamano Dar, makamanda wajifungia ndani

DAR-Sauti za baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA) Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zimenaswa kupitia makundi yao sogosi zimeelekeza lawama kwa makamanda wenzao ambao wameonekana kujifungia ndani wakati wakijua leo Septemba 23,2024 ni siku ya maandamano.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi hao wanaonekana kusikitishwa na hali hiyo huku wakiwataka kutoka ndani ili wakaandamane kupitia njia walizokubaliana awali.

"Habari za asubuhi makamanda, hapa Magomeni Mapipa hali ni shwari kabisa, hakuna polisi yoyote hapa ambaye nimemuona wala hakuna gari lao lolote hapa ambalo nimeliona.

"Kwa hiyo, mpaka muda huu wa saa mbili na nusu hapa hali ni shwari ila watu ndiyo siwaoni,sijui watu mmejificha wapi? Wala sijui mko wapi.

"Mnazi Mmoja hapa nako ni kweupe kabisa, hakuna...hakuna gari la polisi, wala hakuna viashiria vyovyote vile vya polisi,"amebainisha mmoja wa viongozi hao ambaye sauti yake ipo.

Hata hivyo, jitihada za kuwatafuta wahusika ili kupata ufafanuzi zaidi zinaendelea na kadri watakavyotoa ufafanuzi tutawahabarisha.

"Labda wawe askari kanzu, kwa hiyo nimemaliza kufanya patrol kwenye hii njia yangu ambayo ndiyo ambayo nipo ya Magomeni kwenda Mnazi Mmoja.

"Sasa, ninarudi Magomeni kwenye kituo changu, makamanda tokeni ndani, tokeni ndani acheni kulala, acheni. Tokeni huko ndani,"ameongeza Kiongozi mwingine ambaue naye sauti yake ipo.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya watu ambao walidai ni wanachama wa chama hicho akiwemo Said Juma mkazi wa Magomeni Mapipa, Mariam Ally mkazi wa Ilala Boma, Justice Isaya mkazi wa Tabata Bima na Vero Isaya mkazi wa Mbezi Juu wamesema, kwa sasa maandamano si suluhisho la changamoto wanazoziona.

"Kama kiongozi wa nchi hii, Rais Samia Suluhu Hassan ametupa nafasi ya kukaa meza moja mara nyingi kwa ajili ya kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazotukabili. Tunaandamana ili kupata nini?.

"Hao viongozi wetu wa chama waache kutuchosha, kwanza tuna mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya maendeleo ya familia zetu,"amesisitiza Vero Isaya.

Naye Said Juma amesema, mifumo inayotumiwa na viongozi wao kwenda kushinikiza Serikali ifanye mambo si sahihi.

"Wanafanya hivyo ili kuwafurahisha wafadhili au kwa minajiki gani?. Serikali imetupa uwanda mpana wa kuyafikia maridhiano kupitia kukaa pamoja na kujaduliana na si kuandamana,"amesema Juma.

Mariam Ally yeye amesema, hawezi kuunga mkono maandamano kwa sababu anayeumia mara nyingi ni watu wa hali ya chini.

"Kuwa kwangu CHADEMA si kigezo cha kukubaliana kila kitu, kwa hiyo maandamano siyaungi mkono na wala siwezi kuandamana kamawe. Hao viongozi wetu watafute namna ya kukaa na Serikali wajadiliane na kutafuta ufumbuzi wa hayo wanayodhani hayo sawa,"amesema Mariam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news