Watanzania wote wabunifu sajilini bunifu zenu BRELA-Waziri Dkt.Jafo

DAR-Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amewataka wabunifu wote nchini kulinda bunifu zao kwa kuzisajili kisheria ili zisichukuliwe na watu wengine na kujinufaisha nazo bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Wito huo ameutoa leo Septemba 9,2024 katika ziara aliyoifanya ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) jijini Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi na kujifunza namna Wakala inavyotoa huduma za Sajili mbalimbali.

Akizungumza katika kikao hicho,Dkt. Jafo amebainisha kuwa kuna bunifu nyingi ambazo zinachukuliwa na na watu wengine wanaziendeleza na kujiongezea kipato lakini wale wabunifu hawanufaiki na chochote kwa kuwa hawakuzisajili.
“Ninatoa wito kwa watanzania wabunifu wote kusajili bunifu zenu kupitia BRELA maana taasisi hii inakazi ya kulinda haki za ubunifu ili kuwawezesha kufaidika na jitihada za ubunifu na hatimaye kuongeza kipato kwa wabunifu na taifa kwa ujumla,” amesisitiza Dk. Jafo.

Ameeleza kuwa, Tanzania imesaini mikataba na nchi mbalimbali katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Soko Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) katika maeneo hayo yote Watanzania wanashiriki katika biashara mbalimbali hivyo kuna haja kubwa ya wabunifu kutambua haki zao ili zisichukuliwe na wenzetu hivyo niwaombe Watanzania kusajili bunifu zao.
Amewaelekeza watumishi wa BRELA kuwa wawezeshaji wa Wafanyabiashara kwa kuwasaidia katika kufanikisha kurasimisha biashara zao na siyo kuwa kikwazo. Aidha, amewataka kutumia kanuni na sheria kusaidia biashara kwenda mbele na sheria ambazo zinakwamisha ziwasilishwe ili ziweze kufanyiwa maboresho. Ni muhimu kuelewa jukumu la BRELA ni kujenga misingi na mazingira mazuri ya biashara.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, Prof. Neema Mori, amesema kuwa BRELA imedhamiria kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini yanakuwa bora zaidi kwa kuwawezesha, kuwarahisishia na kutoa usaidizi wa karibu kwa wafanyabiashara wanapo rasimisha biashara, kutoa elimu pamoja na kuwahusisha wadau mbalimbali ili wajue namna.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema kuwa,kwa sasa sera ya miliki ubunifu inaelekea kupitishwa na baadaye kuwa na sheria ambayo itasaidia ongezeko kubwa la maombi ya ulinzi wa bunifu hizo ambapo kuna jitihada ambazo BRELA inaendelea nazo katika kuhakikisha elimu ya miliki bunifu inafahamika kuanzia ngazi ya shule ya za msingi hadi vyuo vikuu.

Mbali na jukumu la kusajili miliki ubunifu na utoaji wa hataza amesema kuwa BRELA inatoa ufadhili wa Shahada ya Uzamili ya Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa watu watano kila mwaka ambapo elimu hii mtu atakayoipata itasaidia katika ukuaji wa sekta ya miliki bunifu nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news