Wavulana Wavulana

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, wavulana kwa wasichana bila kujali umri wao, rangi au dini au hali zao wana haki ya kuishi maisha bora na kulelewa katika malezi bora na wazazi wao.
Picha na Parentmap.

Rejea katika maandiko matakatifu, Biblia katika Kitabu cha Zaburi 127:3 kinatukumbusha kuwa, "Tazama,wana ndio urithi wa BWANA, Uzao wa tumbo ni thawabu."

Kwa msingi huo, ni wajibu wa wazazi kwa maana ya baba na mama kuwapa watoto wao maelekezo na kuwarudi kwa namna ya malezi bora tena yanayompendeza Mungu.

Siku za karibuni imeibuka dhana katika baadhi ya jamii kuona kuwa upande mmoja unahitaji uangalizi zaidi kuliko mwingine.

Hivyo, kulifanya kundi la watoto wa kiume kujikuta katika hali ya huzuni na hata kukabiliwa na mashambulizi ambayo yamekuwa yakiacha makovu makubwa maishani mwao.

Tuzingatie kuwa, ni wajibu wa wazazi kuwapa watoto wao malezi yatakayowandaa kuishi maisha bora ambayo hayana majuto huko mbeleni.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakazia kuhusu malezi huku akibainisha kuwa,wavulana wanapaswa kuinuliwa sawa na wasichana. Endelea;

1. Ni waraka kwa wazazi, na watoto wa kiume,
Ya kwamba mnayo kazi, ili wao wasimame,
Kazi yenyewe malezi, hizi nyakati zisome,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

2. Maisha ya siku hizi, sisi sote tujipime,
Nani wapata malezi, wa kike na wa kiume?
Nani wafundishwa kazi, ili kesho wasimame?
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

3. Kimataifa ni wazi, machapisho tuyasome,
Msimamo uko wazi, si kificho tuusome,
Wahitajio malezi, watoto gani tuseme,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

4. Watoto yao malezi, ilo sawa tuiseme,
Chini mitano ni wazi, wanasemwa wasizame,
Baada ya hapo wazi, wa kike si wa kiume,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

5. Yale mambo ya uzazi, si watoto wa kiume,
Msisitizo ni wazi, wale wapigiwa shime,
Lafanyika waziwazi, wala hilo lisikome,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

6. Wavulana wameachwa, acha namba wazisome,
Siyo wao wameachwa, hili budi tuliseme,
Ni kizazi kimeachwa, ili mwishowe kikome,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

7. Majukumu familia, yao wote tuyaseme,
Miaka inapotimia, chansi zao wasimame,
Kutumikia dunia, kama hasa wanaume,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

8. Kwamba jinsi wanakua, wale nini wanaume,
Nini wapaswa kujua, familia isimame,
Nini waweza fukua, waishi na wasizame,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

9. Nafasi yao ni ipi, hasa hasa wanaume,
Yakiwasibu ni wapi, nao waende waseme?
Ni vipi nao wakopi, na kufanya wajitume,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

10. Dunia hii ni yetu, wa kike na wa kiume,
Hivyo ni wajibu wetu, wote hao wasimame,
Ya kwamba kizazi chetu, kidumu na kisizame,
Wainue wavulana, sawa nao wasichana.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news