Wazazi timizeni wajibu wenu katika malezi ya watoto-Naibu Waziri Sangu

NA LUSUNGU HELELA

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amewataka Wazazi kutimiza jukumu la malezi ya Watoto badala ya kuwaachia walimu pekee yao kutokana na wimbi kubwa la mmonyoko wa maadili linaloikumba jamii.Amesema,malezi ya wazazi kwa watoto ni muhimu sana hususan katika nyakati hizi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu katika mahafali ya 37 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kibakwe wilayani humo.
Amesema kitendo cha jumla ya wanafunzi 80 kuacha shule kati ya wanafunzi 247 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021 kutokana na sababu za utoro na mimba, hii inaonesha kuwa kuna baadhi ya wazazi hawawajibiki ipasavyo.

"Leo jumla ya watoto 157 wanahitimu kidato cha nne huku tukiwa tumepoteza watoto 80 kutokana na tatizo la utoro na mimba za utotoni, hii sio sawa Wazazi liangalieni hili.

"Elimu ndo msingi wa kila kitu ukiamua kuwa mfanyabiashara ni lazima uwe na elimu ukitaka kuwa mjasiriamali ni lazima uwe na elimu ndo maana Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anahakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wowote," amesisitiza Mhe.Sangu.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Sangu amewataka wazazi kujiepusha na tabia ya kuwaozesha mabinti katika umri mdogo badala yake wahakikishe wanakumbatia elimu itakayowaandaa kwa ajili ya kupambana na maisha.

Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu amesema Serikali inatarajia kuwapangia vituo vya kazi jumla ya Walimu 247 katika Mkoa wa Dodoma hususan katika Wilaya ya Mpwapwa kutokana na tatizo kubwa la uhaba wa walimu unaoikumba wilaya hiyo.
Amesema, walimu hao watapelekwa katika Wilaya mbalimbali ikiwemo Mpwapwa hivi karibuni ikiwa ni kati ya ajira 11015 za walimu zilizokuwa zimetangazwa na Ofisi ya Rais, Sekretariet ya Ajira mwezi Julai mwaka huu.

Amesema Serikali ya Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu imejipambanua kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora ndio maana anafanya kila liwekanalo kuhakikisha suala la uhaba wa walimu katika shule mbalimbali nchini linakuwa historia.
Aidha, Mhe.Sangu ameipongeza shule hiyo kwa mikakati ya kufuta daraja la nne na sifuri ambapo wamefanikiwa kwa kiasi cha hali ya juu jambo ambalo kwa miaka miwili iliyopita hakuna waliopata daraja la nne na sifuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news