RUVUMA-Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe (MB) amepeleka tabasamu kwa wananchi wa Lwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma baada ya kurejesha hekta zaidi ya 3,000 kati ya hekta 6,580 za shamba la Serikali kwa wakulima.
Waziri Bashe amesema, anatambua shamba hilo lina siasa nyingi,lakini ni lazima kufanya maamuzi magumu kwa maslahi ya wananchi ambao wana haki ya kumiliki shamba hilo.
Akizungumza mwisho mwa wiki wilayani humo katika muendelezo wa ziara yake,Waziri Bashe amesema, wananchi wa Kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo wana haki ya kumiliki shamba hilo.
“Iwapo kuna mwenye hoja awasiliane na mimi, haiwezekani wananchi hawa wakose maeneo na wachache watake kujimilikisha wanavyotaka wao.“Shamba hili lilikuwa la wananchi wakalitoa kwa Serikali chini ya NAFCO ambao walilitumia kwa miaka nane kisha kulitelekeza na baadaye kurudishwa Wizara ya Kilimo na Kilimo tumelitoa kwa Wakala wa Mbegu ASA,limekuwa katika mgogoro kwa zaidi ya miaka 20 huku wananchi wakiwa hawana ardhi ya kilimo.
"Mimi ndio Waziri wa Kilimo naitwa Hussein Bashe nilishatoa maamuzi nasisitiza ekari 3,000 wapewe wananchi na ekari 3,580 zitengwe kwa ajili ya mbegu.
“Watu hawa ni waungwana sana si busara wananchi ambao walijitolea ardhi yao kuwa watumwa nafahamu wapo wachache wanaotaka kujimilisha na kuwafanya wenye haki kuwa manamba,”amesema.
Amesisitiza haja ya uongozi wa wilaya, ASA na wananchi kushirikiana katika uwekaji wa mipaka kati ya ekari za wananchi na ekari za mbegu, ili kusiwepo na mizozo itakayoendelea na kuimarisha ushirikiano kwa jamii hiyo.
Amesema, haoni haja ya kuwapo kwa mgogoro katika ardhi hiyo,kwani wanufaika wa mbegu zinazokwenda kuzalishwa ndio hao wakulima.
“Shamba hili lilikabidhiwa Wizara ya Kilimo na serikali imeona si vyema tukalichukua shamba lote, wakati wananchi wanahitaji ardhi, natoa maelekezo kamati ya ulinzi na usalama, uongozi wa ASA na wataalamu wa wizara undeni timu mkishirikisha wawakilishi wa wananchi, mmkasimamie ugawaji wa shamba na kila mwananchi apate kipande chake katika ekari 3,000 ekari 3,580 zitabaki ASA na wananchi muheshimu mipaka kati yenu na ASA,”amesema Bashe.
Waziri Bashe ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zimewezesha Wizara ya Kilimo kufikisha huduma mbalimbali kwa wakulima ikiwemo ruzuku ya Mbegu na Mbolea, ujenzi wa Maghala, zana za kilimo pamoja na huduma za ugani.
Ameeleza kuwa, pia Serikali imedhamiria kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku nchini, ambapo fedha zitatolewa moja kwa moja lengo likiwa ni kuwawezesha kuzalisha tumbaku yenye kukidhi viwango na mahitaji ya soko la dunia.
Waziri Bashe amewahakikishia wakulima hao kuwa Wizara imeweka mpango mkakati wa upatikanaji wa soko la tumbaku ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo, Vita Kawawa,ameishukuru serikali kwa kazi kubwa inayofanya sekta ya kilimo hususani katika utoaji wa ruzuku za pembejo.