Waziri Bashe awasomea ramani wanaolangua wakulima, Serikali yaja na neema kwao

RUVUMA-Serikali imetangaza kujenga vituo vya zana za kilimo nchi nzima na kuanza kugawa ruzuku ya mbegu za mahindi.
Pia,Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe (MB) amesena atakula sahani moja na wafanyabiashara vishoka wanaonyonya wakulima.

Ameyabainisha hayo leo Septemba 19,2024 katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi akiwa mkoani Ruvuma katika kituo cha ununuzi wa mahindi Madaba.

Amesema,Serikali inatambua adha wanayokutana nayo wakulima kutokana na uhaba wa zana za kilimo, na maumivu wanayokutana nayo katika kukodi trekta,trekta ndogo ikiwemo ulanguzi katika mbegu na mbolea.
Waziri Bashe amesema, Serikali katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija na kufika masoko ya kimataifa na kuifanya sekta hiyo kuinua uchumi imeamua kuwekeza.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa nia ya dhati kabisa ameamua na kutenga fedha za kujenga vituo vya zana za kilimo zaidi ya 45 nchi nzima,”amesema.

Ameeleza katika vituo hivyo kutakuwa na zana za kilimo kama matrekta na zana zake zikiwemo rotavator, plough, cultivator, tractor trailer, harrow, mulcher,planters,boom sprayers na combine harvester.
Waziri Bashe ameitaja mikoa itakayonufaika na awamu ya kwanza ya ujenzi huo kuwa ni Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga, Kigoma, Mara, Tabora,Singida, Katavi,Mbeya, Njombe, Ruvuma, Tanga, Dodoma.

“Tumetambua kuwa wakulima wanakodishiwa zana hizo kutoka sh. 60,000 hadi 120,000 hii ni sawa na kuumiza wakulima na hawawezi kuona tija katika kilimo,Serikali imeamua italeta zana hizo ikiwemo matrekta na wakulima watakodi kwa bei elekezi ya shilingi 35,000 hadi 40,000 haitazidi hapo,”amesema.
Amesema,mwakani pia serikali itasambaza mashine za kusafishia mahindi, mtama na mazao mengine lengo ni kuona bidhaa hizo zinakidhi viwango vya soko la kimafaifa na itatenga fedha ya kununua nafasi zisizo na ubora kwa ajili ya chakula cha mifugo ili kuwapungizia hasara wakulima.

Pia ameeleza lengo la serikali kuanza kutoa ruzuku katika bei ya mahindi.“Tunajua mapambano yaliyopo soko la kimataifa niwahakikishie tunaleta ruzuku katika bei ya mbegu za mahindi, ili kupambana na uhuni unaoendelea.

“Kuna watu wanapaka rangi katika mbegu za mahindi na kuziweka sokoni, tutaondoa mbegu zote ambazo hazikidhi,”amesema Waziri Bashe.

Pia ametangaza vita na wafanyabiashara wanaowanyonya wakulima hususani wanaonunua mazao kwa bei ya chini na wanaouza pembejeo za kilimo kwa bei ya ulanguzi.
“Wapo wafanyabishara wanaonyoya na kula jasho la wakulima bila uoga bei elekezi ya mahindi ni shilingi 700 kwa kilo, lakini wao wananunua kwa shilingi 300, mpunga kilo moja ni shilingi 900 na kilo 100 shilingi 81,000 wao wananunua kilo moja kwa shilingi 600 hii hatutakubali.

“Sina tatizo na wafanyabishara, lakini sitavumilia unyonyaji uliopitiliza tutajenga maghala kila sehemu hawataki kununua naiagiza Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuhakikisha inanunua mazao hayo nchi nzima mpaka kabla na msimu wa kilimo kuisha,”amesema.
Naye Mbunge wa Madaba, Dkt. Joseph Mhagama akizungumza kwa niaba ya wananchi, ameishukuru serikali kwa hatua zinazo endelea, ikiwepo ujenzi wa ghala kubwa katika kata ya Madaba na ujenzi wa vituo 9 vya zana za kilimo mkoni humo.

“Sisi Madaba tumejiandaa kupokea neema hiyo na tumetenga zaidi ya hekari 25,000 za ardhi kupisha eneo la zana za kilimo na mashamba ya mbegu,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news