Waziri Bashe uso kwa uso na Mpina jimboni Kisesa

SIMIYU-Waziri wa Kilimo, Mhe.Husein Bashe (Mb) leo Septemba 13,2024 amefika katika Jimbo la Kisesa lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu na kukutana ana kwa ana na Mbunge wa jimbo hilo,Mheshimiwa Luhaga Mpina.
Waziri Bashe akiwa jimboni humo wakati wa kufunga mashindano ya michezo mbalimbali ya Mwandoya ambapo alipokelewa na mamia ya wananchi amemtaka mbunge huyo kuacha siasa katika zao la pamba.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan inahitaji kuona fedha zinazotengwa zinanufaisha wakulima.

Pia, Waziri Bashe amewaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa, Serikali inarejesha kitalu cha mbegu, kuwapatia ruzuku ya dawa za wadudu katika zao la mahindi na pembejeo zikiwemo mbegu katika zao la pamba.
Katika hatua nyingine, wazee wa kimila katika Jimbo la Kisesa wamemsimika, Mheshimiwa Bashe kuwa Chifu wa jimbo hilo.

“Rais Samia amefanya kazi kubwa katika kilimo, Mpina amesema hapa na mimi nataka nisisitize tuweke mambo mengine pembeni, aache siasa na sitaki siasa katika zao la pamba.

"Nafahamu zipo changamoto, lakini tulipotoka sio tulipo, sitakubali mtu arudishe nyuma jitihada hizi wanaoteseka ni wananchi,”alisema.
Aidha, Waziri Bashe amekabidhi trekta 40 kwa jimbo hilo na kuwataka maafisa kilimo na ugani kuacha kukaa mjini na kuishi vijijini ili waweze kuwasaidia wakulima utaalamu na kufikia malengo ya Serikali ya kilimo chenye tija.

Vilevile amewashukuru wazee wa kimila kwa kumsimika kuwa Chifu wa jimbo hilo.“Nami leo nimesimikwa kuwa Mtemi wa Kisesa, hivyo Mpina akinitambia pale bungeni kwa kuingia na fimbo ya uchifu nami nitaingia na yangu,”amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kennan Kihongosi amemuhakikishia Waziri Bashe kuwa yeye ndiye mwenye dhamana na mkoa huo, hivyo hawezi kuvumilia watu wanaotafuta umaarufu katika siasa kuingiza masuala ya maendeleo.
“Nimetumwa kazi na Rais Dkt.Samia, Simiyu ni ya kwanza ama ya pili katika kuzalisha pamba,hivyo kwa wananchi ni zao la kiuchumi sitaki wanasiasa watumie zao hilo kutafuta umaarufu shida zinazosemwa katika zao hilo si za kweli wananchi wa Kisesa msikubali kutumika,”amesema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina ametumia fursa hiyo kumkaribisha Waziri Bashe jimnoni Kisesa na kueleza kuwa, wanazo tofauti zao, hali iliyowafikisha hadi mahakamani,lakini yupo tayari kushirikiana naye katika masuala ya utendaji wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news