RUVUMA-Waziri wa Madini,Mhe.Anthony Mavunde amepiga marufuku biashara ya madini kufanyika majumbani kwa watu na kusisitiza kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili kudhibiti utoroshaji madini na upotevu wa mapato ya Serikali.
Katika hatua nyingine,Waziri Mavunde amepiga marufuku wafanyabiashara raia wa kigeni kwenda kununua madini machimboni badala yake wafanye shughuli za biashara zao kwenye masoko rasmi na si vinginevyo kwa kuwa ni kinyume na Sheria ya Madini Sura ya 123.
Amesema hayo leo Septemba 17, 2024 wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo kukagua miradi na maendeleo ya shughuli za madini.

Mhe. Mavunde ametoa maelekezo ya kuhakikisha biashara yeyote ya madini kufanyika katika eneo moja na rasmi (One Stop Centre) na kwamba Soko hilo lina mifumo bora na miundombinu yanayotakiwa kwa mujibu wa Sheria.

“Nitoe maelekezo hapa, ni marufuku biashara yeyote ya madini kufanyika nje ya Soko la Madini, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara ya madini kwa uwazi ili kudhibiti mapato ya Serikali, kukuza sekta, na kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa.
“Tutaleta kikosi kazi (task force) hapa na kufanya operesheni maalum ya kudhibiti na kuwabaini watu wote wanaofanya biashara za kununua madini majumbani ili wakafanye shughuli zao kwenye Soko rasmi la madini, na tutachukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaokaidi agizo hili,"ameongeza Mhe. Mavunde.
Amesema kuwa, kwa mfanyabiashara yeyote atayekamatwa akifanya biashara ya madini majumbani atafutiwa leseni yake, madini hayo yatataifishwa na hataruhusiwa tena kufanya shughuli za madini popote nchini Tanzania.

Awali, akiwasilisha taarifa ya Ujenzi wa Soko hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,Bw.Chiza Malando amesema ujenzi wa Soko hilo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.1 hadi kukamilika kwake, wafanyabiashara wakichangia shilingi bilioni 1.085 huku halmashauri ikitoa eneo na ramani yenye thamani ya shilingi bilioni 1.065 kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini,Mhe. Hassan Zidadu Kungu na Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini,Mhe. Daimu Mpakate wameishukuru Serikali kwa usimamizi mzuri Sekta ya Madini na kwamba lengo ni kuona rasilimali ya madini inaleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.