Waziri Mavunde awataka Watanzania kuchangamkia fursa manunuzi ya bidhaa ya shilingi trillioni 3.1 migodini

DAR-Waziri wa Madini,Mheshimiwa Anthony Mavunde amewataka watanzania wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya madini kuchangamkia fursa kubwa iliyopo ya manunuzi ya bidhaa na utoaji huduma migodini. Ni ambayo kwa mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya shilingi trilioni 3.1 zimetumika katika eneo la manunuzi ya bidhaa na huduma.
Waziri Mavunde ameyasema hayo Septemba 13,2024 jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Watoa Huduma na Wasambazaji wa bidhaa Migodini (TAMISA).
“Uwekezaji nchini Tanzania kwenye sekta ya madini unakua siku hadi siku na hii inatokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Chama hichi kitasaidia kuwa na sauti ya pamoja katika kuwajengea uwezo watanzania na kuwaimarisha ili kuwa shindani katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa migodini.
"Natamani sana kuziona hizi Trilioni 3.1 zinabaki mikononi mwa watanzania ili kuchochea uchumi wa nchi yetu kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa na huduma zenye mahitaji makubwa migodini.

"Ninawapongeza sana TAMISA kwa kupokea na kuyafanyia kazi maagizo yangu ya uanzishwaji wa chama hiki cha watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa migodini,ni mategemeo yangu kwamba mtakuwa jukwaa zuri la mafanikio ya sekta binafsi Tanzania,”amesema Mavunde.
Akitoa maelezo ya awali,Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa amesema, chama hicho kina malengo mahsusi ya kuwaleta pamoja watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa migodini,kuishauri Serikali namna bora ya kuwajengea uwezo watanzania kunufaika na sekta ya madini na kushirikiana na serikali kutatua matatizo ya msingi kwenye suala la Local Content.
Akitoa salamu za sekta binafsi,Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TPSF na Mwenyekiti wa Kongani ya Huduma, Octavian Mshiu amepongeza hatua ambazo Serikali inazichukua kwa sasa kuvutia uwekezaji na kukuza sekta binafsi nchini na kuahidi kwamba TPSF itakuwa bega kwa bega na wadau wote kuhakikisha watanzania wanachangamkia uchumi wa madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news