DODOMA-Waziri wa Afya,Mhe. Jenista Mhagama amezindua huduma saba katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) hivyo kuendelea kuimarisha huduma za afya.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma hizo, amepongeza watumishi wa Hospitali kwa ubora wa huduma ya afya.
"Nimpongeze Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Prof. Abel Makubi, na timu nzima ya watumishi wenzake kwa huduma nzuri na ufanisi katika kuboresha huduma," amesema Waziri wa Afya wakati wa uzinduzi wa huduma hizo.
Katika uzinduzi huo, Waziri Mhagama, amezindua maabara maalumu (skills lab) ambayo itawajengea ujuzi wahudumu wa Afya Kanda ya Kati na mikoa ya jirani.
Waziri Mhagama pia amezindua, vyumba maalumu vya upasuaji vinavyotembea (mobile theatre truck) kuwawezesha wataalamu kufanya upasuaji hata mbali na BMH.
Huduma ya tatu iliyozinduliwa na Mhe. Jenista Mhagama ni pamoja na kituo cha huduma kwa mteja (Call Centre) kwa BMH ili kurahisisha mawasiliano kati ya BMH na wateja wake.
Huduma nyingine aliyozindua ni vyumba vipya vya upasuaji vitatu hivyo kufikisha vyumba 11 na hivyo kuongeza wigo wa huduma ya upasuaji kwa BMH.
Waziri Mhagama pia amezindua Miongozo ya Matibabu (SOPs), Huduma kwa Wateja wa BMH, Miongozo ya Idara ya Kutoa Huduma, Kujiendesha na Kujenga uendelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Prof Abel Makubi, amesema watumishi wa Hospitali wameshirikishwa katika kuandaa Standard Operating Procedures (SPOs).
"Niwasifu sana watumishi wangu wa BMH wameshiriki kikamilifu katika kuandaa SPOs ambazo zitatuongoza katika kutoa huduma," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Dkt. Deodatus Mtasiwa, amesema kuanzishwa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni kutokana na muhtasari wa Hospitali kama saba za India, hivyo ndiyo tukaja na BMH.
"Hata mchoraji wa Hospitali hii ni mtanzania baada ya kuangalia muhatasari wa Hospitali saba za India," amesema Dkt Mtasiwa.