MWANZA-Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka Wakufunzi wa uandaaji wa Mtaala wa ufundishaji juu ya masuala ya ndoa za utotoni kutumia lugha nyepesi ya Kiswahili ili Mtaala huo uweze kutambulika na kufahamika kwa haraka.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akisaini kitabu cha wageni baada ya kufika katika ofisi ya Mradi wa Hapana Marefu Yasiyo na Mwisho jijini Mwanza hivi karibuni katika picha ni baadhi ya wasimamizi wa Mradi huo.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa ziara ya Kamati Tendaji ya Mradi wa "Hapana marefu yasiyo na mwisho" walipofika katika Makao Makuu ya ofisi ya Mradi huo huko Mkoa wa Mwanza.
Alieleza kwamba ni vyema kuzingatia lugha ya Taifa katika masuala mbalimbali ya ndani ya nchi ikiwemo uandaaji wa mitaala, kwani itasaidia kila mmoja atakaehitaji kuusoma aweze kuufahamu kwa urahisi.
“Ziara hii inalengo la kuona namna gani Wakufunzi hao walivyoandaa muongozo wa Mtaala kwani ni vyema kuzingatia lugha ya Taifa katika masuala mbali mbali ya ndani ya nchi ili kila mmoja kuusoma, kuufahamu kwa urahisi na kusaidia kuwaelimisha wengine katika jamii”
Sambamba na hayo Mhe. Riziki amewashauri Wakufunzi hao kuwa wanapoandika masuala ya imani ya dini ndani ya mtaala huo, kuhakikisha kunakuwepo uwiano na kuepuka utofauti ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kwa jamii juu ya suala la kupinga ndoa za utotoni.
Pia ameshauri katika mtaala huo uwazingatie na watoto wa kiume kwani nao ni watoto na wanaopaswa kufundishwa masuala mbali mbali ya kujitambua pamoja na kuelimishwa athari za ndoa za utotoni.
Aidha amewapongeza viongozi wa dini walioshiriki katika Mradi huo huku akiwaomba kuitumia vizuri nafasi waliyoipata kwani mtaala huo utakapofanikiwa watakuwa wametoa sadaka kubwa mbele ya Mola wao.