Waziri Ridhiwani Kikwete awahimiza vijana kushiriki kikamilifu uchaguzi wa Serikali za Mitaa

MWANZA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amehimiza vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 2024.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na vijana wa Halaiki mara baada ya kukagua na kujionea maandalizi ya vijana hao walipo watembelea katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza Septemba 26, 2024.
Mhe. Ridhiwani ameyasema hayo leo Septemba 26, 2024 jijini Mwanza wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya vijana ikiwamo wasanii, wanamuziki, waigizaji, wamachinga na waandishi wa vitabu katika ziara yake mkoani humo ya kukagua maandalizi ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.

"Vijana wenzangu jitokezeni mkagombee nafasi hizi sio za watu fulani sisi ndo tunaojua mahitaji yetu kama vijana, hivyo hakikisheni mnajiandikisha kwenye daftari la wapigakura ili kuweza kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa tukachague viongozi bora," amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete wa nne kutoka (kushoto) akifuatilia vijana wa Halaiki wakati akikagua maandalizi ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2024 katika uwanja wa CCM Kirumba, leo Septemba 26, 2024. Wa tano kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Tabia Mwita, wa tatu kutoka (kulia).
Vilevile, Mhe. Ridhwani amehamasisha vijana hao kushiriki katika maadhimisho ya wiki la vijana kitaifa yatakayofanyika jijini Mwanza kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2024 ili kujionea shughuli zinazofanywa na vijana wenzao, taasisi na wadau wanaoshughulikia masuala ya maendeleo ya vijana. Sambamba na hayo amesema kuwa wiki hiyo itaambatana na kongamano la vijana ambalo litashirikisha vijana kutoka Tanzania Bara na visiwani.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ridhiwani Kikwete amekagua maendeleo ya vijana wa halaiki katika uwanja wa CCM Kirumba yatakapofanyika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024; uwanja wa Furahisha itakapofanyika wiki ya vijana na Kanisa la Nyakahoja Parokia ya Mtakatifu Fransisco Xavier (Jimbo kuu la Mwanza) itakapofanyika ibada ya maalumu ya kumuombea Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete akieleza jambo viongozi na wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 wakati walipotembelea Kanisa la Nyakahoja Parokia ya Mtakatifu, Fransisisco Xavier, Jimbo kuu la Mwanza, itakapofanyika ibada maalumu ya kumuombea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Kikwete aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Mwita, Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya masuala ya vijana Zanzibar, Fatma Rajab, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Eliakim Mtawa na Mkurugenzi wa Vijana Zanzibar, Shaib Mohamed.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa tatu kutoka kulia) akimsikilza Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, Emil Kasagara alipotembelea eneo hilo la Furahisha kwa lengo la kukagua maandalizi ya Maadhimisho ya wiki ya vijana Kitaifa yanatarajiwa kuanza Oktoba 8 hadi 14, 2024 Mkoani Mwanza ambapo vijana kutoka Tanzania bara na visiwa watashiriki katika wiki hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news