ZANZIBAR-Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar imeahidi kuendelea kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) katika kuwapatia wananchi fursa zitakazoweza kuwasaidia kujikwamua kimaisha na kuwajengea uwezo ikiwa ni ya chachu ya maendeleo yaliokusudiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma wakati akiwa katika ziara katika Chuo cha Wajasiriamali Wanawake (Bare foot Collage) kilichopo Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema,lengo la ziara yake ni kujifunza pamoja na kuona jitihada zinazofanywa na wanawake katika jamii, hivyo wizara itaendelea kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) katika kuwapatia wanawake fursa na kuondokana na ugumu wa maisha.
Amesema kwamba,kila mwanamke ni kiongozi katika familia, hivyo Serikali itaendelea kuwaunga mkono wanawake na kuwashauri wajasirimali wanawake kutovunjika moyo na kuzikabili changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao, kwani hakuna mafanikio yasiokuwa na changamoto.
Aidha, Mhe.Riziki amewaomba wanaume kuwaruhusu wake zako kwenda kujifunza shughuli za ujasiriamali,kwani kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wanawake kutokupewa ruhusa na waume zao hali hiyo inayowarudisha nyuma kuleta maendeleo katika jamii.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Wajasiriamali Wanawake (Bare foot Collage),Bi.Brenda Godfrey Ndossi amesema, taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wanawake ambao hawana ujuzi wowote ili kuweza kuona wanakuwa na uwezo wa kuzisaidia jamii zao.
Kwa upande wake mwezeshaji katika kituo hicho,Bi.Miza Juma Othman ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwawekea mazingira mazuri ya kuwakomboa wanawake kimaisha ambapo ameiomba Serikali kuendelea kuwaunga mkono wanawake hao waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Nao miongoni mwa wanafunzi waliopatiwa ujuzi, Fatma Haji Machano kutoka Shehia ya Zingwezingwe ameshukuru kupatiwa elimu hiyo pamoja na kutoa wito kwa wanawake wengine ambao hawana kazi wala ujuzi kujiunga na kituo hicho ili kuondokana na umasikini.
Kituo cha Wajasiarimali Wanawake (Bare foot) kina wanafunzi 21 ikiwemo Wazanzibar 12 na Wasomali 9 wanaojifunza utengenezaji wa taa za kutumia umeme wa jua.
Pia, kinatoa ujuzi wa fani tofauti ikiwemo ufugaji nyuki, ushonaji na elimu ya kilimo na tayari kimeshatoa jumla ya wanafunzi 1,054 katika fani tofauti.