WMA:Vitabu vitakatifu vimehimiza vipimo sahihi,pimeni kwa mizani zilizo sawa

NA GODFREY NNKO

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umewataka wanaofanya biashara mbalimbali nchini kunyooka kwa kutumia vipimo halali,kama ilivyo himizo la vitabu vitakatifu na Sheria ya Vipimo ili kumlinda mlaji na kuepuka udanganyifu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla ameyasema hayo leo Septemba 11,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya waandishi wa habari na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Ukihisi mafuta uliyowekewa, ukihisi mtungi wa gesi unaotumia kwa mwezi matumizi hayaendi sawa, tupeni taarifa, hivyo hivyo katika maduka na masokoni ukihisi ulichonunua hakiendani na vipimo halisi tupeni taarifa WMA."

Kihulla amesema kuwa,vitabu vitakatifu ikiwemo Qur'an Tukufu na Biblia Takatifu vimetoa mahimizo muhimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo. Ametolea mfano katika Kitabu cha Amosi 8:5.

Neno la Mungu linasema, "Wakati mwezi mpya utakapoisha, hivyo tunaweza kuuza mazao tena? Wakati siku ya Sabato itakapoisha, ili kwamba tuuze ngano? Tutafanya kipimo kidogo na kuongeza bei, tukidanganya kwa mizani za udanganyifu."

Pia, Mika 6:10-11,Mithali 11:1, 16:11,20:10,23 pia Kumbukumbu la Torati 25:13-16, Warumi 19:35-36 maandiko hayo yote yanazungumzia kuhusu vipimo.

Rejea katika maandiko ya Qur'aan Tukufu; Sura: 83: 1 – 3 Ole wao wapunjao; Sura 17: 35 Pimeni kwa Mizani zilizo sawa; Sura 57: 25 Mizani haki; Sura 55: 7 – 9 Msidhulumu katika Mizani,Sura 42: 17 Mizani haki;
Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ni mojawapo ya wakala za Serikali ambayo ilianzishwa Mei 13,2002 kwa Tangazo la Serikali namba 194 la Mei 17,2002 na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na.340 na mapitio yake ya mwaka 2002.

Kihulla amesema kuwa,miongoni mwa majukumu ya WMA ni kumlinda mlaji na umma kwa ujumla kupitia uhakiki na udhibiti na vipimo vinavyotumika katika biashara na huduma nyingine.

Pia, kuhakikisha vipimo hivyo ni sahihi na vinatumika kwa usahihi kulingana na Sheria ya Vipimo Sura ya 340 mapitio ya mwaka 2002 na maboresho yake ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake.

Katika Sekta ya Biashara, WMA inafanya uhakiki wa vipimo katika maeneo ya biashara kama maduka ya kuuzia nyama, viwandani, mizani inayotumika kuuzia bidhaa masokoni.

Sambamba na bidhaa zilizofungashwa ili kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa kwa usahihi kulingana na thamani ya fedha inayotolewa.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho.

Aidha, kwa upande wa Sekta ya Kilimo, amesema WMA inafanya uhakiki wa mizani zote zinazotumika wakati wa ununuzi wa mazao mbalimbali kama zao la pamba, korosho na ufuta.

Uhakiki huo wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika na kampuni zinazonunua mazao hufanyika kabla ya msimu kuanza ili kujiridhisha kama inatumika kwa usahihi.

Amesema, taasisi hiyo ambayo ilianza kama idara katika Wizara ya Mambo ya Ndani na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara katika sekta ya maji,WMA kupitia kituo cha kisasa cha upimaji katika eneo la Misugusugu na ofisi za mikoa inafanya uhakiki wa dira za maji.

Kihulla amesema,mamlaka zote za maji na waagizaji wote hupeleka dira zao kwa ajili ya kuhakikiwa.

Aidha, upande wa Sekta ya Madini,WMA inahakiki mizani zinazotumika kununulia madini na vito vya thamani na migodini katika masoko ya kuuzia madini na wauzaji wa madini (sonara).

Pia, wanatoa ushauri wa kitaalamu kwa Wizara ya Madini mara kwa mara inapohitajika.

Katika Sekta ya Mafuta, WMA inafanya uhakiki katika sekta hiyo tangu yanapoingia nchini kwa njia ya meli ili kuhakiki kiasi cha mafuta yaliyoingia nchini.
Vilevile, uhakiki wa flow meters za bandarini zinazopima mafuta kutoka kwenye maghala, uhakiki wa matenki makubwa ya kuhifadhia mafuta.

Nyingine ni uhakiki wa matenki ya malori yanayotumika kusafirishia mafuta, uhakiki wa matenki makubwa yaliyo chini ya ardhi yanayotimika kuhifadhi mafuta pamoja na uhakiki wa pampu zote za kuuzia mafuta.

WMA katika Sekta ya Afya inafanya uhakiki wa mizani zinazotumika kwenye vituo vya afya ili kutoa uzito sahihi.

Wakati huo huo, Kihulla amesema katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kuchangia zaidi ya shilingi bilioni 7 katika Mfuko Mkuu wa Serikali ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news