Zanzibar yajipanga kuwa na wataalamu wa kutosha katika TEHAMA

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya uongozi wa Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi imesema kuwa, imejipanga kuhakikisha inapata rasilimali watu wa Kada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya kutosha ili kuiwezesha Serikali kuwa na wataalamu wa ndani wenye uwezo wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA ndani ya Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Ikulu,Mheshimiwa Ali Suleiman Ameir (Mrembo) leo Septemba 30, 2024 wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Mheshimiwa Bakar Hamad Bakar ambaye swali lake limeulizwa na Mheshimiwa Fatma Ramadhan Mohamed (Mandoba).

Kupitia,Baraza la 10 katika Mkutano wa 16 wa Kikao cha 13, Mheshimiwa Bakar alitaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wanapatikana Zanzibar.

"Mamlaka katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Serikali ya Mtandao Na.1 ya mwaka 2024 ina wajibu wa kujua mahitaji ya rasilimali watu Kada ya TEHAMA serikalini, kuratibu matumizi ya rasilimali hiyo pamoja na kuwapatia matumizi endelevu."

Amesema kuwa, Serikali imeweka mkakati madhubuti kuhakikisha inapatikana rasilimali yenye ubunifu na inayoendana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanayoendelea kuibuka duniani.

"Mosi, Mamlaka ya Serikali Mtandao imeanzisha mfumo wa kidigitali na usajili wa watalaamu wa TEHAMA serikalini, kwa lengo la kuhakiki na kuthamini viwango vya elimu, ujuzi na uzoefu wa watendaji ili kuiwezesha Serikali kupata matumizi yenye tija na ufanisi kwa watendaji wao.

"Pili, Serikali kupitia Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje kwa maana ya Daispora inatafuta namna bora ya kuwatumia Diaspora hao ili wasaidie katika kukuza ubunifu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

"Tatu,Mamlaka ya Serikali Mtandao imepanga ushirikiano na taasisi za elimu ya juu nchini, kufanya tafiti mbalimbali za TEHAMA pamoja na kuandaa na kuendesha mafunzo ya kukuza weledi na umahiri kwa wataalam wa TEHAMA serikalini.

"Ni imani yangu kwa hatua nilizozitaja hapo juu zinawezesha Serikali kuwa na wataalamu wa ndani wenye uwezo wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA hapa Zanzibar,"amefafanua Waziri huyo.

Kuhusu mpango wa Serikali wa kuwahimiza vijana kusoma masomo ya TEHAMA amesema, Serikali ina mikakati mbalimbali ambayo ni jumuishi na shirikishi kuhakikisha kuwa, kila mmoja anapata fursa kupitia ujuzi na utaalamu wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news