ZFDA yakamata mabegi manne yenye dawa za binadamu

ZANZIBAR-Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) kwa kushirikiana na wakaguzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar (AAKIA) wamekamata mabegi manne yenye dawa za binadamu zilizoingizwa nchini zikitokea India kwa kutumia Shirika la Ndege la Ethiopia bila kufuata utaratibu.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Dawa na Vipodozi, Sabrina Idrissa Ahmada amesema, dawa hizo si salama kwa watumiaji,kwani hazijasajiliwa na ZFDA.

Vilevile ameeleza kuwa,dawa hizo zilifungashwa katika kifungashio kisicho rasmi kusafirishia dawa na muingizaji wa dawa hizo si halali kutokana na kutosajiliwa na kufuata taratibu zilizowekwa.

Sabrina alizitaja baadhi ya dawa hizo kuwa ni pamoja na dawa za kutibu saratani, tenzi koo (goita), magonjwa ya akili na antibiotics.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ZFDA ilieleza kuwa,baada ya kuingia nchini mzigo huo ulishughulikiwa na mtoa mizigo (agent) Nassor Humoud ambaye alidai kutokuwa na maelezo ya kutosha ya mmiliki halali wa mzigo huo baada ya kuhojiwa na wakaguzi hao.

Mbali na hayo Sabrina aliwaomba wadau mbalimbali ikiwemo wa sekta ya afya na vyombo vya habari kushirikiana katika kuhakikisha elimu na miongozo juu ya usalama wa dawa inafika katika ngazi zote za jamii kwa lengo la kulinda afya za watumiaji.

Kufuatia tukio hilo lililotokea Septemba 5, 2024, ZFDA imeziweka dawa hizo chini ya uangalizi na usimamizi maalum na kumtaka mtoaji wa wa mzigo huo (agent) kuwasilisha barua ya kujieleza pamoja na vielelezo vya uingizaji wa dawa hizo, ili taratibu nyingine za kisheria ziendelee kuchukuliwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news