NA LWAGA MWAMBANDE
OKTOBA 14 mwaka 1999 ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe, kwani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St. Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua saratani ya damu.
Mwili wa Mwalimu Nyerere ulipokelewa jijini Dar es Salaam Oktoba 18, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani.
Oktoba 20, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao.
Aidha, Oktoba 21, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria ibada hiyo na watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi Oktoba 22, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya maziko.
Maziko ya Mwalimu Nyerere yalifanyika Oktoba 23, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika Kijiji cha Butiama wilayani Musoma Vijijini Mkoa wa Mara.
Tangu wakati huo hadi leo kila ifikapo Oktoba 14 ya kila mwaka,huwa ni kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa nchini.
Tanzania imeendelea kuadhimisha Siku ya Nyerere ambayo imepewa heshima kubwa si tu kwa sababu alileta Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, bali pia aliweka msingi wa umoja na usawa kwa Watanzania.
Pia, Hayati Baba wa Taifa alikuwa na maono ya taifa lenye mshikamano na usawa kupitia falsafa ya Ujamaa akiweka mbele haki za wanyonge na maendeleo kwa wote.
Vilevile, Mwalimu Nyerere aliamini kuwa Watanzania wangefanikiwa endapo wangeshirikiana na kujitegemea, badala ya kutegemea misaada kutoka nje.
Falsafa hii ilichochea juhudi za kujenga nchi yenye nguvu kiuchumi na kijamii, ambapo kila mmoja alikuwa na nafasi ya kuchangia.
Hata hivyo, zaidi ya kuwa kiongozi wa ndani, Nyerere alikuwa sauti ya Afrika nzima, akipinga ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa kupitia robo karne hii Hayati Baba wa Taifa ataendelea kukumbukwa zaidi, kwani aliyoyafanya wakati wa uhai wake yanaishi. Endelea;
1. Kwetu ni robo ya karne, kukosekana Mwalimu,
Yanadondoka matone, yake jinsi yanadumu,
Twabakie tujikune, jinsi yanavuta hamu,
Alikufa bado hai, alofanya yanaishi.
2. Nyerere ni mwanzilishi, marais twafahamu,
Naye kwa wake utashi, kwa wema alihudumu,
Japo likuwa hachoshi, mwenye aliishiwa hamu,
Alikufa bado hai, alofanya yanaishi.
3. Hivi leo kwetu nani, ambaye twamfahamu,
Kutoka kwake moyoni, kuhudumu asidumu,
Nyerere tunamwamini, aliridhika na zamu,
Alikufa bado hai, alofanya yanaishi.
4. Uhuru Nyerere wetu, alichukua kwa zamu,
Na wale mababu zetu, waliyafanya matamu,
Kujenga taifa letu, tuko sawa wanadamu,
Alikufa bado hai, alofanya yanaishi.
5. Umoja wa nchi yetu, Kiswahili twafahamu,
Yote makabila yetu, yake yangeleta sumu,
Aliongoza mwaketu, kote lugha inadumu,
Japokuwa alikufa, alofanya yanaishi.
6. Huu Muungano wetu, unaishi ni timamu,
Kivyetuvyetu ya kwetu, twatekeleza kwa zamu,
Ni wa aina yetu, vema kwa wema udumu,
Japokuwa alikufa, alofanya yanaishi.
7. Huu wake upekee, anakumbukwa Mwalimu,
Rushwa kote itokee, lakini si kwa Mwalimu,
Mwacheni atokezee, mwadilifu wa kudumu,
Japokuwa alikufa, alofanya yanaishi.
8. Ukombozi wa Afrika, Nyerere alihudumu,
Kotekote asifika, hata katika elimu,
Nasi sifa zinafika, tutokao kwa Mwalimu,
Japokuwa alikufa, alofanya yanaishi.
9. Nasi tuzidi muenzi, huyu Nyerere Mwalimu,
Tuige yake mapenzi, kazi njema kwa nidhamu,
Tusifanye ya ushenzi, yanayoleta wazimu,
Japokuwa alikufa, alofanya yanaishi.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602