Asante sana Mwalimu

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Oktoba 5,2024 ni Siku ya Walimu Duniani ambayo inaongozwa na kauli mbiu ya “Kutambua Sauti za Walimu". Kauli mbiu hii inazingatia umuhimu wa kuwasikiliza walimu na kuwashirikisha katika kuunda sera na mipango mbalimbali ya elimu.
Picha na KU.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Dunia inahitaji walimu wa ziada milioni 44 ili kufikia elimu ya msingi na sekondari kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Aidha,ingawa mahitaji ya walimu ni makubwa zaidi katika baadhi ya maeneo, uhaba wa walimu ni wa kimataifa. Kwani, walimu wanajiondoa kwenye taaluma hiyo kwa kiwango mara mbili zaidi ya miaka mitano iliyopita, hasa katika elimu ya sekondari.

Miongoni mwa sababu zinazochangia ni hali zao za kazi ikiwemo mishahara midogo, mzigo mkubwa wa kazi, na ukosefu wa ushiriki katika maamuzi yanayohusu elimu.

Ifahamike kuwa, walimu wana mchango mkubwa katika kujenga kizazi chenye akili, chenye tabia na kinachoweza kukabiliana na changamoto za siku zijazo.

Licha ya mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kutoa pongezi nyingi kwa walimu,pia ameendelea kusisitiza kuwa, Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si Dunia. Endelea;

1. Popote pale ulipo, unayeitwa Mwalimu,
Pokea salamu ulipo, siku hii ya Walimu,
Twaenzi wako uwepo, jinsi watupa elimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

2. Mwalimu wewe ni dawa, hilo vema ufahamu,
Ujinga tukichachawa, wasafisha usidumu,
Mambo tunayoelewa, mchango wako Mwalimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

3. Leo twaiadhimisha, siku ya kwako Mwalimu,
Twazidi kukuvumisha, kwamba udumu Mwalimu,
Uzidi tuelimisha, maujinga yasidumu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

4. Kusoma na kaundika, metufundisha Mwalimu,
Ufundi twachakarika, ni kazi yako Mwalimu,
Twazidi kuerevuka, mchango wako Mwalimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

5. Kuanzia chekechea, upo na sisi Mwalimu,
Msingi twaedelea, sekondari ni Mwalimu,
Shahada twazipokea, asante kwako Mwalimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

6. Sisi tusio walimu, tujue kuna Mwalimu,
Yake vema tufahamu, aishi vema Mwalimu,
Hakize tusidhulumu, achokechoke Mwalimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

7. Kumsumbuasumbua, apate shida Mwalimu,
Mengi tunayatibua, katika yetu elimu,
Vema tukatambua, na kumuenzi Mwalimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

8. Hii siku ya Mwalimu, vema tukamhudumu,
Ajue tunafahamu, ule wake umuhimu,
Na ya kwamba tutadumu, tukimuenzi Mwalimu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

9. Leo kote duniani, anaenziwa Mwalimu,
Malawi hadi Japani, aadhimishwa Mwalimu,
Ile ya kwake thamani, kutambulika yadumu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

10. Mesota sana Mwalimu, tukapata ufahamu,
Asante sana Mwalimu, pokea zetu salamu,
Kutufundisha udumu, kwani ujinga ni sumu,
Dunia bila Mwalimu, ingekuwa si dunia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news