Baa zote ambazo hazina mifumo ya kuzuia sauti Zanzibar zapigwa marufuku kupiga muziki

ZANZIBAR-Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni Zanzibar limezuia upigaji wa muziki katika baa zote za Zanzibar ambazo hazina mifumo maalumu ya kuzuia sauti (sound proofs) ili kuepusha usumbufu kwa jamii.
Katibu Mtedaji wa Baraza hilo, Chum Juma Chum amesema, hatua hiyo imekuja baada ya kupata maalamiko kutoka kwa jamii juu ya upigwaji huo wa muziki na kusababisha kero.

Amewaeleza wanahabari kuwa, baraza limesitisha utoaji wa leseni za muziki kwa kumbi za baa hadi pale zitakapokidhi vigezo na masharti ikiwemo sehemu ya kudhibiti sauti.

Hata hivyo baraza linaendelea kufanya ziara ya ukaguzi katika maeneo yote ya kumbi za burudani kwa lengo la kudhibiti athari zinazotokana na kelele za muziki kwa jamii.

Hivyo alizitaka taasisi na jamii kwa ujumla kufuata sheria na taratibu za baraza hilo ikiwemo ukataji wa leseni ili kuepusha kufungiwa na endapo watakiuka sheria hizo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumzia kuhusu shughuli za kijamii amesema, utaratibu utaendelea kama kawaida kwa kufuata maelekezo ya vibali vinavyotolewa na masheha wa maeneo husika.

Naye Mrajis wa baraza hilo, Abdillahi Ramadhan Nyonje amesema,baraza kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama watafanya zoezi la ukaguzi wa baa zote ili kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza katika baa hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news