Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yawataka wahitimu kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya Fedha

MWANZA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amewataka wahitimu wapya wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania kutumia maarifa na ujuzi waliopata kwa uadilifu na weledi ili kusaidia kuimarisha sekta ya fedha nchini.
Akizungumza katika Mahafali ya Tatu ya Chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 31 Oktoba 2024 jijini Mwanza, Gavana Tutuba alisisitiza kuwa sekta ya fedha ni mhimili wa uchumi wa taifa, hivyo inahitaji wataalamu waaminifu wenye maadili na ujuzi wa hali ya juu.

“Nawasihi kutumia elimu na ujuzi mlioupata kulitumikia taifa letu kwa weledi, uadilifu na uzalendo mkubwa. Muwe kioo na tunda la Benki Kuu ya Tanzania, na kuwa mfano bora kwenye sekta ya fedha,” alisema Gavana Tutuba.
Aliongeza kuwa Benki Kuu inafuatilia kwa karibu wafanyakazi wote wa sekta ya fedha na haitasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya wizi au udanganyifu.

Akizungumza kuhusu changamoto za ajira kwa vijana, Gavana Tutuba alihimiza wahitimu kuwa wabunifu, wachapakazi, na kutumia ipasavyo ujuzi waliopata. 

Alisema mfumo wa kujifunza wa vitendo unaotumika chuoni hapo unawapa wahitimu uwezo wa kukabiliana na ushindani wa ajira na pia kuwajengea uwezo wa kujiajiri. “Ujuzi huu utawasaidia sana katika kuingia kwenye soko la ajira na kujiajiri,” aliongeza.
Aidha, Gavana aliwasisitizia wahitimu umuhimu wa kujiendeleza kitaaluma na kitaalam kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na uchumi duniani. 

Alisema mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi, na kiteknolojia, pamoja na ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia ya nchi, yamefanya iwe muhimu kuendelea kujifunza na kupata maarifa mapya.

“Kuhitimu kwenu siku ya leo kuwe ni chachu na mwanzo wa safari mpya ya kujifunza na kupata maarifa mapya katika maeneo na viwango mbalimbali,” alisema.

Akizungumza awali, Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Dkt. Nicas Yabu alieleza kuwa katia kuboresha sekta ya fedha nchini, zaidi ya watoa huduma ndogo za fedha 1,280 wamepata mafunzo kupitia programu maalum ya muda mfupi (Crush Programme), huku wahitimu 103 wakitunukiwa vyeti vya umahiri kwenye sekta hiyo.
Dkt. Yabu aliongeza kuwa chuo kinaendelea kutoa mafunzo ya usimamizi wa sarafu, ambapo wahitimu 83 wamepatiwa vyeti vya umahiri. 

Pia, chuo kimefanikisha kutoa cheti cha umahiri kwa watoa elimu ya fedha kwa umma 97, ili kusaidia kukuza uelewa wa masuala ya kifedha kwa wananchi.

Katika jitihada za kuimarisha zaidi sekta ya mikopo, Dkt. Yabu alisema kuwa chuo kwa sasa kinakamilisha mtaala wa cheti cha umahiri kwa maafisa mikopo kwa kushirikiana na Taasisi ya Mabenki Tanzania (TIOB).

“Mtaala huo utapitiwa na wadau mwezi Novemba 2024, na kwamba programu hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwaka 2025, hatua itakayosaidia kuwajengea maafisa mikopo ujuzi na weledi unaohitajika katika sekta hiyo,”alisema.
Katika mahafali hayo, wahitimu 40 wamekutunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki (Ordinary Diploma in Banking Practice and Supervision) na wahitimu 38 wametunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki (Postgraduate Diploma in Banking Management).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news