MWANZA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo ya Uongozi wa Kimkakati kwa viongozi wa taasisi mbalimbali za kifedha ili kuwajengea uwezo wa kuongoza taasisi zao kwa umahiri na ufanisi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoratibiwa na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Benki Kuu na Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani, Bw. Julian Banzi Raphael, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kukuza maarifa, ujuzi, na mtazamo unaohitajika kuongoza taasisi za fedha kimkakati na kwa ufanisi katika mazingira ya biashara yenye changamoto na mabadiliko mengi ya sasa.
“Mafunzo haya yatawawezesha viongozi kutumia fursa zilizopo, kufanya maamuzi sahihi, kukuza utamaduni wa maboresho endelevu na uwezo wa kubadilika, na kuhamasisha wengine kufikia mafanikio ya muda mrefu," alisema.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatajaa mijadala ya kina na ushirikiano wa kivitendo kati yao, ambayo mwishowe itakuza uwezo wao wa utendaji.
“Mtajadili Uongozi wa Kimkakati na Kuongoza Mabadiliko ya Kimkakati; Mawasiliano ya Kimkakati kwa Utendaji Bora; na Usimamizi Bora wa Timu. Vipengele hivi vyote vina mchango mkubwa katika utendaji wa taasisi" aliainisha.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Benki Kuu Mwanza, Profesa Tadeo Satta, alibainisha kuwa mafunzo hayo yameshirikisha wawakilishi kutoka Benki za Biashara za hapa nchini, pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, Ghana, Zambia, Zimbabwe, na Burundi.
Profesa Satta alifafanua kuwa mafunzo haya yana lengo la kubadilishana uzoefu, mawazo, na utaalamu kuhusu namna bora ya kuendesha sekta ya fedha kwa ufanisi.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na uongozi madhubuti katika sekta ya fedha ili kuimarisha uchumi wa nchi. “Bila kuwa na viongozi wenye weledi wa kimkakati, ufikiaji wa malengo muhimu ya sekta hii utakabiliwa na changamoto,” alisema Profesa Satta.
Mafunzo hayo yanayoongozwa na kauli mbiu “Kiongozi wa kimmkakati anainua motisha na tija ya wafanyakazi inayopeleka utendajikazi mzuri wa Shirika,” yanayofanyika katika Chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza kuanzia tarehe 28 hadi 30 Oktoba 2024.