GEITA-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuja na bunifu mbalimbali ambazo zinalenga kuwamilikisha nyumba bora wananchi kote nchini.
Miongoni mwa bunifu hizi ni pamoja na mpangaji mnunuzi ambapo mwananchi anaweza kumiliki nyumba aliyopangisha kwa shirika huku akilipa fedha kidogo kidogo hadi atakapokamilisha malipo yake.
Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Ahmad Mwangu ameyasema hayo leo Oktoba 12,2024 wakati akizungumza katika Maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili mkoani Geita.
"NHC tumekuja kushiriki katika maonesho haya kwa ajili ya kuwaletea fursa wananchi mbalimbali wa Geita na mikoa jirani ili wapate fursa ya kuziona bidhaa zetu ambazo tunazitoa NHC.
"Tuna miradi ya aina mbalimbali, tuna miradi ya kipato cha chini, cha kati na cha juu.Na miradi yetu ipo katika mikoa mbalimbali ambayo tunaitekeleza, lakini pia NHC tunatekeleza miradi zaidi ya kujenga nyumba na kuuza, tunashiriki katika miradi ya ukandarasi au ya usimamizi wa miradi na mambo mengine."
Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Ahmad Mwangu akizungumzia kuhusu nyumba za kipato cha chini ambazo wanazo katika mikoa mbalimbali hapa nchini amesema.
"Kwa mfano hapa Bombambili mkoani Geita tuna nyumba za kipato cha chini (affordable housing) na nyumba hizi zipo katika mpango maalum wa ulipaji, tumegawa katika vipindi vitatu jinsi ya kulipa. Tuna ulipaji wa miaka mitano, miaka kumi na miaka kumi na tano.
"Nyumba hizi za hapa zinagharimu shilingi milioni 49 kwa nyumba ya vyumba viwili na ile ya vyumba vitatu inagharimu kama shilingi milioni 72.
"Nyumba hizi,tumeita kwa mtindo wa mpangaji mnunuzi kwa maana nini? Kwamba unapanga unapokuwa unalipa pango la kila mwezi na hapo unakuwa unalipa gharama ya ununuzi kwa nyumba.
"Kwa mfano kodi ya hapa ni shilingi 150,000 lakini utaongeza gharama ya ununuzi wa nyumba ambapo utajipatia nyumba hizi kwa bei nafuu kabisa.
"Kwa hiyo baada ya kutanguliza asilimia 10 ya malipo ya awali, pesa inayobaki utalipa kwa kipindi hicho nilichosema cha miaka mitano, kumi na kumi na tano."
Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Ahmad Mwangu amesema, kwa utaratibu huo mwananchi wa kawaida anaweza kumiliki nyumba hiyo kwa gharama nafuu.
"Kwa mfano, nyumba ya shilingi milioni 49 ambayo kwa miaka 15 unaweza kulipa 42,500 kwa mwezi.
"Mfano rahisi tu kama unaweza kupata shilingi 15,000 kila siku katika mizunguko yako na biashara na kazi zako.
"Elfu kumi na tano ukiilipa kwa siku 30 maana yake ni shilingi 450,000 kwa hiyo unaweza kujikuta unanua nyumba yako kwa shilingi elfu kumi na tano kila siku.
"Kwa laki nne na nusu kwa mwezi na kwa miaka 15 utakuwa umemalizia asilimia 100 ya gharama zako,"amesema Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Ahmad Mwangu.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kufika katika banda lao lililopo viwanja vya Bombambili ili kuweza kupata fursa ya kufahamu miradi mbalimbali wanayotekeleza.
Miradi hiyo amesema ipo katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma huku pia Arusha wanauza viwanja kwa ajili ya ujenzi.
Tags
Habari
Mikoa ya NHC
NHC Tanzania
Sera ya Ubia NHC
Shiri la Nyumba la Taifa (NHC)
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)