DAR-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amepongeza jitihada za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kuhakikisha wananchi wanafikishiwa Nishati Safi ya Kupikia.
Ametoa pongezi hizo Oktoba 23, 2024 jijini Dar es Salaam alipotembelea Banda la REA katika Kongamano la 10 la Jotoardhi (ARGeo-C10).
Aidha ameielekeza REA kutazama namna ya kuweka ruzuku kwenye majiko yanayotumia nishati ya umeme kama inavyofanyika kwenye mitungi ya gesi na majiko banifu ili kuwawezesha wananchi wamudu gharama.
Alisema kwakuwa umeme umefika kila kona ya Nchi ni muhimu pia REA ikaandaa mpango maalum wa ruzuku katika majiko yanayotumia nishati ya umeme.
"Mmefanikisha kuweka ruzuku kwenye mitungi ya gesi na majiko banifu, mtazame namna ya kuwa na ruzuku kwenye majiko haya ya umeme ili kila mwananchi mwenye kuhitaji aweze kumudu gharama yake," alielekeza Mhe. Dkt. Mpango.
Awali akitoa maelelezo ya majukumu ya REA, Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya alimueleza Makamu wa Rais, Mhe. Mpango kuwa Wakala unatekeleza programu mbalimbali ili kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilima 80 ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia kama inavyoelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034).
Mhandisi Yesaya alisema Wakala umeingia makubaliano na wasambazaji wa mitungi ya gesi ambayo tayari inatolewa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 katika mikoa yote Tanzania Bara ambapo kwa awamu ya kwanza mitungi ya 452,445 inatolewa.
Aidha, alifafanua kuhusiana na ruzuku ya hadi asilimia 75 ambayo itatolewa katika majiko banifu ambapo alisema kwa kuanzia, takriban majiko 200,000 yatatolewa kwa bei hiyo ya ruzuku