Faraja ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC ni kuona kila mpangaji anaishi kwa raha, lakini uzingatie haya

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah amesema, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 ankara za kodi za nyumba zilizopokelewa kwa wateja zilifikia kiasi cha shilingi bilioni 101.38 na shirika likakusanya shilingi bilioni 106.86 sawa na asilimia 105.40.
Ameyasema hayo leo Oktoba 13,2024 katika mkutano wa viongozi wa Jimbo la Ilala mkoani Dar es Salaam ambapo alikuwa anaelezea mafanikio na mizania ya shirika kwa mwaka 2023/2024.

Sambamba na kuelezea mwelekeo wa shirika kwa mwaka 2025 katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-25.

"Maana yake tulivuka malengo ya ukusanyaji wa kodi zetu, tumeongeza ufanisi katika ufuatiliaji, lakini vile vile wapangaji wetu wameanza kutambua wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati. Lakini, kama shirika tuna madeni ambayo tunaendelea kuyakusanya."

Pia, amesema katika kipindi cha Julai 2023 shirika lilikuwa na deni la pango shilingi bilioni 24.9. "Hadi kufikia mwezi Juni 2024 shirika limekusanya deni la shilingi bilioni 4.8 na juhudi mbalimbali zinaendelea kukusanya deni lililobaki."

Amesema, shirika lina zaidi ya shilingi bilioni 27.2 za wapangaji kama fedha za amana ya pango ambazo hutumika pale mpangaji anapoacha deni.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, huwa hajisikii faraja kuona mpangaji anatolewa katika nyumba kwa kushindwa kulipa kodi au kwa kushindwa kutimiza masharti ya upangaji wa nyumba.

"Kwa sababu usimwangalie tu yule baba ambaye ndiye kiongozi kwenye ile familia, kuna kina mama watateseka, kuna watoto watateseka.

"Lakini, kuna kadhia kadhaa ambazo wanazipitia, kwa hiyo siku zote nimekuwa nikiwaambia hata watendaji wangu jamani tujitahidi sana tuwahimize na kuwakumbusha wapangaji wetu walipe kodi kwa wakati.

"Tusiwavizie kwa ajili ya kuwatoa,lakini tusimuonee mpangaji kama anatimiza wajibu wake, hii ninaizungumza kwa sababu tunarekebisha na toka tumeanza hizo kampeni kuna wapangaji ambao walikuwa na madeni makubwa tuliwaambia waje ndani ya shirika.

"Badala ya kuwatoa tuingie nao mkataba ambao utawafanya wawe wanalipa kodi ya kila mwezi wakati huo huo wakipunguza sehemu ya madeni yao,na inafanya vizuri.

"Pale ambapo mpangaji haoneshi ushirikiano kabisa ndipo ambapo tunachukua hatua za kumtoa kwa sababu kuna maelekezo ya kisheria na ya kimkataba kufanya hivyo,lakini si jambo ambalo tunapenda kulifanya.

"Kwa hiyo, madeni yetu tunayakusanya tunaingia mikataba na wapangaji wetu kwa ajili ya kulipa hizo kodi na sehemu ya madeni yao, lakini vile vile ili kuondokana na hiyo kadhia na matakwa ya kisheria tumeweka kitu tunaita amana ya pango.

"Ambayo wapangaji wetu wengi wameweza kuilipa ambayo hii sasa inatuondoa kwenye ile dhana ya kuwatoa watoa wapangaji kwa sababu tayari tuna amana yao."
Pia, amewaeleza kuwa, mpango wa matengenezo wa nyumba za shirika umeanza kwani kuanzia mwaka wa fedha huu majengo mengi yameanza kuwa na muonekano mpya.

"Tumeanza, lakini vile vile mwaka huu wa fedha tuna shilingi bilioni 15 ambazo tunaendelea kutengenerza hizo nyumba, nyingi hazipo katika hali nzuri, lakini tumeendelea na maboresho ya hizo nyumba ili wapangaji wetu waweze kuishi katika maeneo mazuri."

Wakati huo huo amesema kuwa, shirika linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukandarasi na ushauri elekezi, ujenzi wa nyumba za makazi za gharama nafuu na kati, uboreshaji wa miji kwa kuvunja majengo ya zamani na kujenga mapya.

Amesema kuwa,miradi mengine ni upangaji wa miji na uendelezaji vitovu vya miji, uendelezaji wa miji kwa njia ya ubia.

Katika miradi ya ukandarasi amesema,shirika linatekeleza miradi nane ya majengo ya Serikali Mtumba jijini Dodoma yenye thamani ya shilingi bilioni 186 inayotarajiwa kukamilika Januari 31, 2025.

Aidha,miradi mengine ni ujenzi wa shule maalumu Mbuye Chato mkoani Geita ambao umegharimu shilingi bilioni 5.5 na umefikia asilimia 96.

Sambamba na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kwangwa Musoma mkoani Mara ambao umegharimu shilingi bilioni 15.1 na umefikia asilimia 100 ikiwemo miradi mingine mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news