Hakuna atakayeachwa nyuma huduma jumuishi za kifedha-Gavana Tutuba

NA GODFREY NNKO
Zanzibar

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, ifikapo mwaka 2028 wanatarajia Watanzania zaidi ya asilimia 85 watakuwa wamefikiwa na huduma jumuishi za kifedha nchini.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 1,2024 na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba muda mfupi baada ya ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Mwaka wa Kamati ya Mamlaka za Usimamizi wa Bima,Masoko ya Mitaji na Huduma za Fedha zisizo za Kibenki (CISNA) jijini Zanzibar.
Mkutano huo ambao ulianza Septemba 29, 2024 huku ukitarajiwa kutamatika Oktoba 4, 2024 umefunguliwa na Mheshimiwa Ali Suleiman Ameir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, Zanzibar kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba.

"Sisi kwa umoja wetu tumekuwa tukishirikiana kwa pamoja na tunaendelea vizuri, tumewezesha kwa ujumla kiwango cha Financial Inclusion kwa Tanzania kimefikia asilimia 76 kulingana na utafiti wa Fiscal Study uliofanyika mwaka jana 2023.

"Lakini, tuna mpango wa kufikia asilimia 85 ifikapo 2028, kwa hiyo tunapoona jitihada kama hizi kwamba sisi ni sehemu ya jamii inayosimamia masuala ya fedha.

"Hivyo tunao wajibu wa kuendelea kushiriki na kutoa mchango wetu kwa kadri itakavyowezekana tuhakikishe gurudumu hili la kutoa elimu na kutoa huduma za kifedha kwa makundi yote liweze kufikiwa haraka kadri iwezekanavyo, kama ilivyo lengo moja wapo kwenye jumuiya yetu ya SADC."

Gavana Tutuba amesema, kulingana na utafiti huo wa mwaka jana kuna baadhi ya maeneo yanayoonekana kuwa yalibaki nyuma, hivyo wameendelea kuyafanyia kazi ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika huduma jumuishi za kifedha.

"Kuna maeneo makuu matano, eneo la kwanza ni eneo la wanawake ambao wapo nyuma katika ufikiwaji wa kifedha, kundi la pili ni watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

"Eneo la tatu ni vijana hususani wa chini ya miaka 18 au wale waliomaliza shule ambao hawajapata kazi rasmi."

Gavana Tutuba amesema kuwa, eneo la nne ni la wakulima wadogowadogo na eneo la tano ni la wa wavuvi, kwa hiyo hayo maeneo yamebainishwa.

"Lakini, kwa ujumla wake tukaona kwamba, changamoto inayowakabili ni kiwango cha chini cha elimu ya fedha, kwa hiyo sisi Benki Kuu kwa kushirikiana na wadau wengine tumetengeneza miongozo mikubwa miwili.

"Wa kwanza ni masuala ya Financial Literacy,tumetengeneza muongozo wa kutoa elimu kwa watu ambao wako ndani ya mifumo rasmi ya shule au elimu.

"Na ule muongozo tunashukuru, tumekutana kwenye kikao cha Baraza la Huduma Jumuishi za Kifedha cha Kitaifa, walipitia na kuridhia ambapo mimi pia ndiye Mwenyekiti.

"Lakini, ule muongozo ulishaanza kutumika kwa upande wa Tanzania Bara, Wizara ya Elimu walishauchukua, wameufanyia kazi."

Gavana Tutuba amesema,kwa upande wa Tanzania Zanzibar pia, Wizara ya Elimu waliuchukua na wameshaingiza kwenye mitaala ya shule za msingi, sekondari na vyuo.

"Wanaendelea kuutumia ili kuuingiza kwenye ile mitaala, utakuwa ukitumika sasa rasmi."

Gavana Tutuba amesema, muongozo wa pili ni ule wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi (Out of Schools Curriculum).

"Sasa, muongozo ule nao, sisi kama Benki Kuu tumeutumia kwa kuhamasisha watu ili watakapofahamu masuala mbalimbali ya kifedha wanaweza kuendelea kuutumia na ikawa ni sehemu ya maisha yao."

Amesema, ukilinganisha na nchi za wenzetu, hapa nchini bado elimu ya fedha ipo chini."Ndiyo maana tulikuja na mkakati huo, japokuwa tuna mikakati mingine inayoendelea itakayotuwezesha kufikia hilo lengo la asilimia 85 au hata zaidi.

"Kwa upande wa Tanzania Bara tuna mikakati ya kuwezesha coverages ya umeme kufikia asilimia 100 vijiji vyote ifikapo mwaka 2025."

Amesema, wananchi wakishafikiwa na huduma za umeme watakuwa na fursa ya kutumia simu na huduma nyingine za kifedha ambazo zitakuwa zinapatikana mitandao.

"Lakini,kuna mkakati mkubwa wa kuwezesha ipatikane intaneti kwa nchi nzima ifikapo mwaka 2025, tunafahamu kwa mfano kwa Tanzania Bara kuna makampuni mengi yanayojenga minara.

"Kuna makampuni tu yanaendelea kutandaza Mkongo wa Taifa ili ufike kila kona nchini, sasa hiyo itakuwa ni fursa ya kuwezesha hiyo intaneti ipatikane."

Gavana Tutuba amesema, kupitia mikakati hiyo na mingine wanaamini ifikapo mwaka 2028 tutakuwa na hizo huduma jumuishi za kifedha kwa watu wote.

"Na kama tukifikia hiyo asilimia 85 au zaidi sisi tutakuwa bado tupo vizuri kwa sababu tutashirikiana na wadau wengine."

Katika hatua nyingine,Gavana Tutuba ametoa wito kwa watu ambao hawajafikiwa na huduma jumuishi za kifedha kuendelea kuangalia fursa zilizopo na kuzitumia vizuri.

"Kwa kufanya hivyo, watapata manufaa yao wenyewe. Tumeendelea kutoa elimu kwenye maeneo mbalimbali hasa kwa mfano wastaafu wengi kabla ya kustaafu tumekuwa na majadiliano, tunawapa elimu.

"Ili wakipata hata fedha zao wawekeze kwenye Hatifungani za Serikali na Dhamana za Serikali, tumeendelea kuwahamasisha watu kila wanapopata labda mitaji, basi waiwekee dhamana au waiwekee bima.

"Kata bima uilinde biashara yako,pengine biashara yako itakuwa na uhimilivu na itaendelea kushamiri zaidi.

"Kwa hiyo,kwa mikakati tuliyoweka kupitia maeneo mbalimbali tunaamini kabisa kwa mwaka 2028 tutafikia lengo hilo, ikiwezekana tutakuwa tumevuka na zaidi hasa kupitia teknolojia za kidigitali na products mbalimbali ambazo zinatolewa,"amebainisha Gavana Tutuba.

Mbali na hayo, Gavana Tutuba amesema kuwa,CISNA ilianzishwa chini ya Kurugenzi ya Fedha, Uwekezaji na Forodha ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema,kamati hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kubadilishana kwa taarifa na uzoefu miongoni mwa mamlaka kuhusu masuala ya udhibiti na usimamizi wa masuala ya bima, masoko ya mitaji, pensheni na huduma za fedha zisizo za kibenki.

"Jukumu kuu la CISNA ni kuoanisha kanuni na miundo ya usimamizi ya nchi wanachama na kuhakikisha kuwa zinakidhi viwango vya kimataifa vilivyowekwa na taasisi za viwango za kimataifa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news