NA LWAGA MWAMBANDE
KWANZA ninamshukuru Mungu ambaye ameniwezesha kukamilisha vitabu vitano katika mfululizo wa kutoa vitabu vya mashairi mwaka huu.
Ni kwa neema tu ninaweza kufanya haya yote, pi ninamshukuru mke wangu na watoto wangu kwa kuendelea kuwa msaada mkubwa kwangu.
Vilevile, ninamshukuru Mungu kwa ajili ya Mchungaji Kiongozi wa Moto Ulao Online Church, Mch. Imani Oscar Katana, pamoja na watumishi wa Mungu wote popote pale walipo kutokana na mafundisho ya Neno la Mungu ambayo yamekuwa chachu kubwa sana kwangu kutunga mashairi na hata mengine kuwa katika vitabu hivi.
Ninawashukuru wana MUOC wote kwa ushirikiano mkubwa mnaotoa katika huduma yangu hii ya utunzi wa mashairi. Mungu azidi kuwabariki awawezeshe mfike mbali katika uchaji wenu.
Oktoba 17,2024 kupitia Moto Ulao Online Church (MUOC), vitabu vitano nilivyozindua ni;
1. Hebu kula chuma hicho
2. Chukia hali ya sasa
3. Sadaka ina harufu
4. Cheza na ahadi zako, na
5. Hufungua yagomayo
Kwa muhtasari:
(a) HEBU KULA CHUMA HICHO ni diwani inatukumbusha kwamba changamoto katika maisha haziishi - zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo. Kwa tunaomtegemea Mungu, hatutakiwi kukata tamaa au kuvunjika moyo, bali kukabiliana nazo kwa matumaini kwamba hatuko peke yetu. Mungu yu pamoja nasi.
Hebu kula chuma hicho, kutoka kwa mhusika,
Ni wazi bila kificho, teseka hadi kuchoka,
Changamoto si kichocho, kirahisi chatibika,
Neno ndio ukombozi, kukabili hali ngumu.
Na lingine linasema:
Vyovyote tujiandae, kwa magumu kuteseka,
Lakini tusichakae, kama tutamalizika,
Imani kwetu tujue, alitoka tutatoka,
Neno ndio ukombozi, kukabili hali ngumu.
Mashairi utakayosoma yatakuonesha jinsi Mungu anavyoshughulika na yale yanayokushughulisha hatua kwa hatua. Katika shairi la Mtu anayekufaa, usimwache kirahisi kuna ubeti unasema:
Una mtu wa maana, ambaye anakufaa,
Naye zidi shikamana, yake yazidi kukaa,
Faida utaziona, tena waweza kupaa,
Mtu anayekufaa, usimwache kirahisi.
Karibu ujisomee, uimbe na unufaike…KULA CHUMA HICHO!. Endelea;