Huduma ya maji hakuna atakayeachwa nyuma nchini

DODOMA-Ni mpango uliopigiwa mfano mkubwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” kwa kuhakikisha Tanzania inapata mabadiliko makubwa katika huduma ya maji na kuleta chachu ya mafanikio katika nyanja nyingine za maendeleo ya wananchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika uzinduzi wa mradi wa maji wa Mtyangimbole, Ruvuma.

Oktoba 14, 2024 ilikuwa ni kumbukizi ya baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alipigania maendeleo ya wananchi wote, bila kujali asili yake au eneo alipo.

Kumbukumbu na historia imebaki kwa Rais Samia kutafuna fupa lililoshindikana la mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe ambao ulikaa zaidi ya miaka 15.

Ni mradi uliobeba sifa ya kutokamilika kwa muda mrefu , ila kwa Rais Samia, sasa mradi unafanya kazi na imekuwa historia. Kwa upana mengi yanafanywa na Serikali ili kuleta neema kwa jamii.

Maono hayo, yanaendelezwa na Wizara ya Maji katika kuwaletea wananchi maendeleo , na sapoti kubwa itolewayo na Rais Mhe. Samia hivi sasa amewezesha kila eneo ambalo halijafikiwa, wananchi kuchimbiwa Kisima cha majisafi, kwa maana ya mpango wa kuchimba visima 900, ambao ameuzindua hivi karibuni Ruvuma alipofanya ziara ya kikazi.

Pamoja na hilo wadau wa maendeleo nao wanaunga mkono kazi ya kufikisha huduma ya majisafi kwa wananchi ambapo Novemba 2023 Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Dkt. Victoria Kwakwa akiwa katika mkutano wa viongozi wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika unaohusu masuala ya upatikanaji wa majisafi na salama na usafi wa mazingira nchini Ethiopia aliipongeza Tanzania kwa kutekeleza kwa ubora na viwango Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (PforR) na kuwa kinara kati ya nchi nyingine Duniani zaidi ya 50 zinazotekeleza programu hiyo.

Dkt. Kwakwa kwa maendeleo hayo aliiomba Tanzania kutoa uzoefu wa mafanikio yake katika miradi ya maji na huduma kwa wananchi kwa nchi nyingine za Mashariki na Kusini mwa Afrika ambazo zilishiriki mkutano huo muhimu

Kwa mpango na picha hiyo, hakuna Mtanzania atakayeachwa kwa miradi mbalimbali yam aji inayoendelea, makubwa na midogo.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) anasema kazi mbalimbali zinaendelea katika kila kona ya nchi ili kufikia lengo la upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95.

Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2021 hadi asilimia 77 mwezi Desemba 2023 na kwa upande wa mijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 84 mwaka 2021 hadi wastani wa asilimia 88 mwezi Desemba 2023.

Moja ya mafanikio na kichocheo cha mabadiliko katika Sekta ya Maji ni ushirikishwaji wa jamii katika kufanikisha mahitaji muhimu ya huduma ya maji. Mfano mojawapo ni program ya Mpango wa matokeo ambapo kutokana na ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji kumeleta matokeo bora, Sekta ya Maji awali ilipata dola 350 milioni na ndani ya miaka mitatu ilikuwa imepeleka maji kwa zaidi ya wanufaika wapya maeneo ya vijijini wapatao milioni 4.7.

Juhudi hiyo, Aweso anasema imewezesha wananchi milioni 6.6 kuwa na vyoo bora vijijini katika Mikoa 17 ikiwa ni matokeo makubwa kuliko nchi nyingine Duniani zinazotekeleza mradi kwa Mpango wa Matokeo chini ya Benki ya Dunia (WB).

Pamoja na program hiyo, Wizara ya Maji imejipambanua katika kufanikisha kazi ya kufikisha huduma ya maji katika jamii kwa kutekeleza mambo mbalimbali, kwa kuongeza kasi ya ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika miji 28 ambapo miradi hiyo inalenga kunufaisha wananchi zaidi ya milioni moja katika maeoneo yote ya mradi, na kazi mbalimbali zinaendelea kwa kasi na ufuatiliaji unafanyika mara kwa mara kwa wataalam na viongozi wa Sekta ya Maji.

Jingine ni kuongeza kasi ya ujenzi wa bwawa la Farkwa na mtambo wa kusafisha na kutibu maji ili kuweza kuondoa changamoto ya uhaba wa maji katika Jiji la Dodoma na miji ya Chamwino, Bahi na Chemba;

Kupeleka maji katika maeneo yenye upungufu, ikiwamo kujenga mradi wa kutoa maji ziwa Victoria kupeleka miji ya Singida na Dodoma ili kuondoa kabisa changamoto ya uhaba katika Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi.

Pia, kukamilisha ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo litapunguza uhaba wa maji katika Jiji la Dar es Salaam ambalo ni Jiji la Kibiashara na chanzo kiubwa cha mapato ya Serikali.

kuendelea kujenga miradi mikubwa inayotumia vyanzo vya maji vya uhakika vikiwemo mito mikubwa na maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa; na kutafiti maji chini ya ardhi kwa ajili ya kuchimba visima virefu na kujenga miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi

Kwa ujumla jamii inapaswa kuelewa kuwa maji ni rasilimali muhimu kwa maisha ya binadamu, maendeleo ya kiuchumi na kijamii, pia ni kichocheo muhimu katika shughuli za majumbani, kilimo cha umwagiliaji, mazingira, umeme wa nguvu za maji, viwanda, uvuvi, mifugo, madini na utalii.

Upatikanaji wa maji kwa ajili ya sekta mbalimbali pamoja na usimamizi madhubuti wa rasilimali za maji ni msingi wa shughuli zote za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa usalama wa Taifa. Kulinda vyanzo vya maji na miundombinu ya maji ni muhimu kwa kila mwana jamii ili kupata huduma endelevu ya maji katika ya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news