Jaji Kahyoza afanya ziara ya ukaguzi wa Mahakama za wilaya Kigoma

■Ateta na Watumishi wa Mahakama hizo

■Awasisitiza Mahakimu kutumia Mfumo wa Uratibu na Usimamizi wa Mashauri (e-CMS)

■Wasisitizwa kutozalisha mashauri ya mlundikano

NA AIDAN ROBERT
Mahakama Kigoma

WATUMISHI wa Mahakama za Wilaya Kigoma wamesisitizwa kutumia vema rasilimali fedha zinazopatikana katika kuboresha zaidi huduma za Mahakama kwa kuwa wananchi wanatarajia huduma nzuri na yenye viwango vya juu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza akipanda mti wa mparachichi wakati alipowasili katika Mahakama ya Wilaya Buhigwe kwa ajili ya ukaguzi wa kawaida wa Mahakama za Wilaya, wengine ni viongozi na watumishi wa Mahakama hiyo wakishuhudia zoezi la upandaji wa mti.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama za Wilaya tano za Kasulu, Kibondo, Buhigwe na Kakonko pamoja na Mahakama za Mwanzo akiwa katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama hizo hivi karibuni, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza alisema hatua hiyo ni katika kuhakikisha kuwa, changamoto zilizopo zinatatuliwa kwa haraka ili kuepusha kuzalisha mlundikano wa mashauri katika Kanda hiyo.

Aidha, aliwasisitiza watumishi kufanya jukumu zaidi ya moja pale wanapoona kuwa kuna upungufu wa nguvu kazi, kwakuwa itasaidia kuleta tija katika kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma mahakamani.

“Hakikisheni mnaweka mikakati thabiti ya kumaliza mashauri katika vituo vyenu maana kwa wakati huu Mahakama inapojipambanua katika maboresho ya kiteknolojia ni dhahiri sasa nasi twende kwa kasi hiyo ili tuweze kumhudumia mwananchi kwa viwango vya huduma vinavyokubalika kisheria, miongozo na taratibu za kazi bila kuacha maelekezo ya viongozi hii ndio itatupa thamani kubwa katika utendaji wetu wa kazi,” alisema Mhe. Kahyoza.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (aliyeketi mbele) akiendesha kikao cha watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo wakati alipowasili kwa ajili ya ukaguzi wa Mahakama hiyo. Wengine ni viongozi alioambatana nao pamoja na watumishi Mahakama ya Wilaya Kibondo wasikiliza kwa makini maelekezo ya Jaji Kahyoza.

Pamoja na mengine, Jaji Kahyoza aliwapongeza Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama hizo kwa kuchapa kazi licha ya kuwa na changamoto za kimazingira na upungufu wa watumishi na vitendea kazi. Kadhalika amewapongeza kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa (2020/2021-2024/2025) unaolenga kuboresha huduma za utoaji haki.

Aidha, amewataka kudumisha mahusiano mazuri kazini kwa kupenda kituo cha kazi pamoja na kushirikiana vyema na wadau wote waliopo katika wilaya husika ili kurahisisha utoaji huduma za Mahakama.
Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Kigoma ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akipanda mti wa matunda (parachichi) katika Mahakama ya Wilaya Buhigwe mara baada ya kuwasili mahakamani hapo akiambatana na Jaji Kahyoza kwa ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya.

Aliongeza kuwa, pamoja na maboresho ya Mahakama ya Tanzania ni vema wakatafuta namna ya kufufua Mahakama za Mwanzo Nyaronga na zingine katika Wilaya zote zisizofanya kazi katika maeneo yote ya Mkoa wa Kigoma kwa kuwa miji inakuwa na shughuli za kibinadamu zinakuwa, hivyo huduma za kimahakama katika maeneo hayo ni muhimu kuwepo ili kupunguza umbali uliopo baina ya Mahakama moja na Mahakama nyingine na hatimaye, kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kimahakama.

Jaji huyo aliwakumbusha pia watumishi hao kufanya kazi kwa ubunifu na weledi ili kuboresha zaidi huduma zinazotolewa na Mahakama hizo ili kuleta chachu katika utumishi na kurahisisha huduma kwa mteja wa Mahakama.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (wa kwanza kushoto), wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Katoke Mwakitalu (wa pili kushoto).

Kwa upande wake Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo aliwapongeza Watumishi wa Mahakama hizo kwa kazi nzuri wanazoendelea kufanya katika Mahakama zao na kuwasisitiza kuendelea hivyo pamoja na kudumisha ushirikiano wa kazi ili kuleta tija katika utendaji wa shughuli zao za kila siku katika kuwahudumia wananchi.

“Tuhakikishe hatuzalishi mashauri ya mlundikano na tusiruhusu pia wadau wa Mahakama zetu kuwa chanzo cha mashauri ya mlundikano ni vema sasa kuwashirikisha mikakati yenu mliyojiwekea ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kutekeleza shughuli zetu na hii itatuongezea heshima na picha nzuri ya Kigoma kuwa ya mfano kila wakati huko,” alisema Mhe. Tarimo.
Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu (waliosimama). Wa pili kushoto ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (wa pili kushoto), wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Imani Batenzi na wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Emmakulata Shulli.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Bw. Filbert Matotay aliwapongeza watumishi hao kwa jinsi wanavyojituma kufanya kazi na kushirikiana katika kuleta matokeo mazuri ya kazi.

“Nitashirikiana na uongozi wa Mahakama za Wilaya zote kuhakikisha changamoto za kiutendaji na za kiutumishi zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo katika kuzitatua ili kuendelea kuboresha na kutoa huduma nzuri kwa wananchi katika Mahakama zote Kanda ya Kigoma,” alisema Bw. Matotay.Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe (waliosimama). Wa pili kushoto ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Kigoma ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo, wa kwanza kushoyo ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe.Venance Katoke Mwakitalu na wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Buhigwe, Mhe. Straton Mosha.

Aidha, ameahidi kuendelea kutatua changamoto ya ikama ya watumishi kwa kutambua watumishi wenye uwezo na taaluma tofauti kusaidia maeneo yenye upungufu katika shughuli za Mahakama na kubainisha kwamba, ataendelea kuomba watumishi wapya kadri ya ajira mpya zinapopatikana.
Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Rweyongeza Kahyoza (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko, wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki, wa pili kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kakonko, Mhe. Ambikile Kyamba.

Mhe. Kahyoza alifanya ukaguzi katika Mahakama hizo kuanzia tarehe 24-27 Septemba, 2024 lengo likiwa ni kujua hali ya utekelezaji wa majukumu sambamba na kufahamu changamoto mbalimbali zilizopo ili kuangalia namna ya kuzitatua na hatimaye kutoa huduma bora kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news