Jaji Mkuu ataka Dira ya Taifa 2050 kulindwa kikatiba

NA INNOCENT KANSHA
Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Timu ya wataalam wanaoandaa rasimu ya Dira ya Taifa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ilindwe na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ili iweze kudumu kwa muda mrefu zaidi, kwa kuzingatia maoni ya wananchi mambo yote muhimu yaliyoibuliwa yanapatikana katika Katiba hiyo.
Mkuu wa Timu Kuu ya Wataalam inayoandaa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro (kulia)akieleza kwa ufupi lengo la kukutana na Jaji Mkuu. Picha chini, Balozi Migiro kwa heshima kubwa akionesha ishara ya shukrani kwa kukaribishwa kuzungumza na Jaji Mkuu.

Akizungumza mapema leo tarehe 29 Oktoba, 2024 Ofisini kwake jijini Dar es salaam alipotembelewa na Timu Kuu ya Wataalum inayoandaa Rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayoongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro, Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amesema Dira hiyo ikisimamiwa na sheria za kawaida inaweza kuchezewa na kutotoa matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa maendeleo na ustawi wa Taifa.

“Je Dira hii ikitoka tutaipa nguvu ya aina gani, nguvu ya sheria ya kawaida au nguvu ya kikatiba ili ipate uendelevu zaidi. Kwa sababu ikiwa kwenye nguvu ya sheria ya kawaida inaweza ikachezewa chezewa lakini kutokana na juhudi kubwa zilizofanyika katika kuitengeneza pengine itakuwa vyema ikipewa nguvu zaidi ya kikatiba ili iweze kudumu kwa muda mrefu zaidi,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu akaongeza kuwa mambo mengi ya kimaendeleo yanategemea sana sekta binafsi katika kuleta msukumo wa mabadiliko ya kimaendeleo lakini katika nchi nyingi zinazoendelea Serikali bado ina mchango mkubwa sana. Kwa sababu ni nadra sana kwa sekta binafsi kuingia kwenye uwekezaji mkubwa mathalani ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa mabarabara makubwa, ujenzi wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) lazima kuna maeneo ambayo Serikali inapaswa kuendelea kuwa injini ya mabadiliko.

Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amesema eneo lingine ambalo Dira inapaswa kuliwekea mkazo ni elimu na ujuzi ni lazima elimu itumike kuwa kichocheo cha mabadiliko ‘agent of change’. Mfano; elimu kuanzia Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu inapaswa kuakisi mabadiliko na si kwa kukusanya vyeti tu. Kama elimu hiyo haitaleta mabadiliko ya kifikira dhidi ya kupigania fursa za kimaendeleo hasa katika karne 21 inayotawaliwa na teknolojia ya habari na mawasiliano basi elimu hiyo itakuwa haijakidhi na kujitosheleza.
Mkuu wa Timu Kuu ya Wataalam inayoandaa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro akiongoza mazungumzo hayo.

“Na nadhani hiyo ndiyo changamoto ambayo hata Dira iliyopita ilikuwa inazungumzia kwamba je? tunatumia elimu kama mkakati wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii ama la, ni lazima tuangalie hata nchi za wenzetu kama Ulaya zina ajenda ya kubadilisha ujuzi na kuangalia Ulaya ya miaka 20 ijayo itakuwaje, ni vema nasi tukalizingatia hilo,” ameongeza Mhe. Prof. Juma.

Akiongelea maboresho na mabadiliko ya kimtazamo kwa wananchi ‘Change of mind-set’ Mhe. Prof. Juma amesema ni jambo la msingi la kutazamwa Taifa linaweza kuwa na mipango mizuri na Dira nzuri lakini bila kufanyia kazi mtazamo ‘atitude’ juu ya Dira mpya bado tukawa na watu miongoni mwa jamii ambao wanakizana na uhalisi wa mambo mazuri yatakayo changia kuharakisha maendeleo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na mgeni wake, Mkuu wa Timu Kuu ya Wataalam inayoandaa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro (hayupo katika picha).

“Tunapotengeneza kitu chochote iwe ni sheria ama utawala bora na mitizamo yetu ijikite katika utawala bora, tunaposema utawala wa sheria tusiwe watu wa kuongea tu utawala wa sheria lakini maudhui yetu na shughuli zetu za kila siku zinapaswa kuwa katika misingi ya utawala wa sheria,” amesema Jaji Mkuu.

Awali akiwasilisha msingi wa maoni ya wananchi juu ya Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 Mkuu wa Timu Kuu ya Wataalum inayoandaa Rasimu ya kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro amesema Dira ya sasa imekuwa shirikishi sana tofauti na Dira ya kwanza kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan toka alipozindua rasmi mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 alisisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika uandaaji wa Dira hiyo.
Akitoa mwelekeo wa maudhui na muundo wa Rasimu ya Dira hiyo kutokana na maoni ya wananchi Mhe. Balozi Dkt. Migiro amesema Dira hiyo itabeba mambo mengi yanayohusu maendeleo ya uchumi, tunu za taifa, na kanuni muhimu zinazohimiza ujenzi wa Taifa.

Mhe. Migiro amebainisha malengo makuu matano ambayo yatakuwa msingi wa Dira hiyo kuwa, ni kuzingatia ustawi kwa wote, ilenge kujitegemea kama Taifa, ibebe msingi wa Taifa lenye haki, msingi mwingine ni umoja na mshikamano wa kitaifa na kwa kuwa Tanzania sio kisiwa iwe nchi mshiriki na mshindani muhimu kidunia.
Mkuu wa Timu Kuu ya Wataalam inayoandaa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro (kulia) akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipowasili ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam Leo tarehe 29 Oktoba, 2024.

“Wananchi wameeleza katika maoni yao wanatamani kuona Dira yetu ijikite katika misingi ya utaifa tuwe na watanzania ambao wanazingatia mambo fulani fulani yapatayo 10 ambayo yatatusaidia kujenga utaifa na mambo hayo hayataguswa wala kutikiswa ila jitihada zote zifanyike ziwe za kisheria, za kikanuni na za kisiasa kuyaimarisha na kuyaendeleza,” ameongeza Dkt. Migiro.

Mhe. Migiro amesema mambo hayo kuwa, ni kulinda na kuheshimu utu, kulinda na kudumisha uhuru wa nchi na watu wake, kuwe na usawa wa raia zake na wa nchi, kuwe na uadilifu na uwajibikaji, kuwe na msingi ambao utalinda na kudumisha umoja wa kitaifa, kuwe na uwazi katika uendeshaji wa shughuli za kiserikali na za kijamii, uwazi kwenye matumizi ya rasilimali za taifa, uwazi katika matumizi na faida zitokanazo na rasilimali hizo na jinsi zinavyosaidia ujenzi wa Taifa na maendeleo, ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za Taifa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake, Mkuu wa Timu Kuu ya Wataalam inayoandaa Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Mhe. Balozi Dkt. Asha-Rose Mtengeti Migiro. Picha chini akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Dkt. Migiro pamoja na wataalam wengine alioongozana nao kwenye mazungumzo hayo.

Mambo mengine yaliyoainishwa miongoni mwa mambo 10 ya msingi ni ubunifu kwa kulinda jitihada zinazofanywa na watanzania mmoja mmoja kama vile vijana, wanawake, wanaume katika kuwa wabunifu na hiyo itakuwa ni nyenzo mojawapo ya kujenga utaifa vilevile kujenga mtazamo wa kuona mbali na mtazamo wa kidunia.

Mhe. Migiro akazifafanua nguzo nne zitakazo jenga Dira ya Taifa amesema, mosi ni haja ya kujenga uchumi imara jumuishi na shindani, maendeleo ya watu na jamii hasa rasilimali watu kwa kuagalia elimu inakuwa bora, afya bora kwa wote, makazi bora na usalama wa chakula.Nguzo nyingine ni uhifadhi wa mazingira na utimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia ya nchi hasa matumizi ya ardhi na rasilimali zingine kama vile nishati mbadala na nishati safi na salama zilizopo nchini. 

Nguzo hizo zote zitabebwa na msingi mkuu ambao utakuwa ni uongozi bora, amani, usalama, utulivu na umoja kwa maana nyingine nguzo hiyo itajengwa na masuala ya utawala bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news