Jaji Mkuu wa Tanzania yupo tayari kuchagua viongozi wa Serikali ya Mtaa

NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 17 Oktoba, 2024 amejiandikisha kwenye Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini tarehe 27 Novemba, 2024.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akiwa katika chumba cha kujiandikisha katika Shule ya Msingi Oysterbay Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam leo tarehe 17 Oktoba, 2024.

Mhe. Prof. Juma aliwasili kwenye kituo cha kujiandikishia kilichopo katika Shule ya Msingi Oystebay Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam majira ya saa 9.00 alasiri kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo ambalo linatarajia kutamatika tarehe 20 Oktoba, 2024 kabla ya uchanguzi kufanyika mwezi Novemba.

Serikali ilitangaza ratiba ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa akieleza kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika siku 19 kabla ya uchaguzi.

Mhe. Mchengerwa alieleza pia kuwa endapo kutakuwa na mgombea mmoja pekee kwa nafasi husika, atateuliwa moja kwa moja.

"Upigaji wa kura utaanza saa 12:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni," alisema na kueleza kuwa nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji katika mamlaka za wilaya.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto juu na picha mbili chini) akijiandikisha kwenye Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini tarehe 27 Novemba, 2024.

"Kwa nafasi hizo, uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika mamlaka za Wilaya za mwaka 2024," alisema.

Waziri Mchewngerwa alieleza pia kuwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika mamlaka za miji midogo utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika mamlaka za miji midogo za mwaka 2024.
Alisema uteuzi wa waandikishaji na waandaaji orodha ya wapigakura kwa mujibu wa kanuni hizo, utafanywa na msimamizi wa uchaguzi atakayeteua watumishi wa umma watakaoandikisha na kuandaa orodha ya wapigakura siku 52 kabla ya siku ya uchaguzi.

"Uandikishaji wapigakura kwa mujibu wa kanuni na uandaaji wa orodha ya wapigakura utaanza siku ya 47 kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa muda wa siku 10," alisema.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mwandikishaji wa kati wa zoezi hilo, Bw. Hussein Omary Mohamed.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 145 na 146 inaelezea uwepo wa Serikali za Mitaa pamoja na madhumuni yake. Mojawapo ya madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news