DODOMA-Shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge kwa mwezi Oktoba, 2024 zitaanza tarehe 7 hadi tarehe 25 Oktoba, 2024. Shughuli hizo ni pamoja na vikao vya Kamati kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge unaotarajiwa kuanza siku ya Jumanne tarehe 29 Oktoba, 2024.
Katika kipindi hicho, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) zitatangulia kuanza vikao tarehe 7 Oktoba, 2024.
Kamati zilizosalia zitaanza vikao tarehe 15 Oktoba, 2024. Vikao vya Kamati zote vitafanyika Dodoma na vitaendelea hadi tarehe 25 Oktoba, 2024. Shughuli zitakazotekelezwa wakati wa Vikao vya Kamati za Bunge katika kipindi hicho ni kama ifuatavyo:-
Kuchambua Miswada ya Sheria
Shughuli hii itatekelezwa na Kamati tatu (3) za Bunge ambazo ni Kamati ya Miundombinu, Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
Kuchambua Sheria Ndogo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, itafanya Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Kumi na Sita.
Kupokea Taarifa za Utendaji wa Serikali na Taasisi zake
Kamati kumi na moja (11) za kisekta zitapokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji wa Serikali na Taasisi zake. Aidha, Kamati ya Bajeti itapokea taarifa mbalimbali kutoka Serikalini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Fedha na masuala yanayohusu vyanzo vya mapato ya Serikali.
Kuchambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
Kamati mbili (2) zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, zitachambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Wizara, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa Mwaka wa Fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2023.
Matokeo ya uchambuzi huo yanatarajiwa kuwasilishwa Bungeni na kujadiliwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Saba wa Bunge utakaoanza tarehe 29 Oktoba, 2024.
Kuchambua Taarifa za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma ili kubaini iwapo uwekezaji huo una ufanisi na kwamba, umezingatia taratibu na miongozo mujarabu ya biashara.
Ratiba ya Shughuli za Kamati inapatikana katika tovuti ya Bunge ambayo ni www.bunge.go.tz