ZANZIBAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Mhe. Ali Suleiman Ameir Mrembo amesema, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. DkT. Hussein Ali Mwinyi atazindua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mikutano na makongamano mbalimbali.
Waziri Mrembo ameyasema hayo leo Oktoba 18,2024 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, mbele ya waandishi wa Habari alipozindua rasmi kampeni ya Miaka Minne ya Rais Dkt.Mwinyi pamoja na nembo maalum.
Aidha, Waziri Mrembo ameeleza kuwa kampeni hiyo itaanza rasmi Oktoba 21,2024 hadi Novemba 16, 2024.
Halikadhalika, Waziri Mrembo amesema, kampeni hiyo itawafikia wananchi kupitia teknolojia ya habari, ikiwemo televisheni, mitandao ya kijamii, magazeti, na redio za kijamii.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Ramadhan Bukini, amesema kampeni hiyo itajumuisha Mawaziri na Watendaji mbalimbali wa Serikali, ambao watazungumzia mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kila sekta, kupitia mahojiano yatakayoendeshwa na katika Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).