RUVUMA-Naibu Waziri Nishati na Mbunge wa Viti Maalum Vijana Taifa, Mhe. Judith Kapinga amewahamasisha wananchi katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
Mhe. Kapinga amesema hayo hivi karibuni wakati akifungua Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa Viongozi, Watendaji na Wadau wa Wilaya ya Mbinga.
"Ni muhimu kila mmoja wetu akashiriki zoezi la kujiandikisha, sio kujiandikisha wewe tu bali kuhamasisha na wengine kwenye eneo lako waweze kujiandikisha."
Amesema ili wananchi waweze kuweka viongozi imara watakaofaa kwenye jamii, ni lazima kuwe na watu wengi wa kuwapigia kura, hivyo ni vyema wananchi wakahamasishana ili kwenda kwa wingi kujisajili kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kuchagua viongozi watakaowatumikia kwa weledi na kutatua changamoto mbalimbali pale zinapojitokeza.