Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara aiagiza Menejimenti ya WMA kutekeleza maono ya Rais Dkt.Samia

Ø Akabidhi magari kuboresha utendaji kazi

Ø Azindua Jarida maalum kupanua wigo uhabarishaji umma

NA VERONICA SIMBA
WMA Pwani

KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah ameitaka Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia utendaji kazi wenye weledi, ubora na viwango ili kupata matokeo chanya katika sekta ya biashara nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah (katikati- mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) Alban Kihulla (kulia kwake), Menejimenti na Mameneja wa Mikoa yote Tanzania Bara baada ya kufungua kikao chao kujadili utendaji kazi, Oktoba 3, 2024 Kibaha mkoani Pwani.

Ameyasema hayo kwa waandishi wa habari Oktoba 3, 2024 Kibaha mkoani Pwani baada ya kufungua rasmi kikao cha Menejimenti ya WMA, kukabidhi magari ili kuboresha utendaji kazi na kuzindua Jarida maalum la Wakala lenye lengo la kupanua wigo wa uelimishaji na uhabarishaji umma kuhusu WMA.

“Lengo kubwa la kikao chetu ni kukumbushana wajibu na dhamira nzima ya majukumu yetu ambayo yanatakiwa yaakisi maelekezo na miongozo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala zima la kuwezesha ufanyaji biashara ndani ya nchi yetu.”
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akikata utepe kabla ya kukabidhi magari kwa Wakala wa Vipimo (WMA) ili kusaidia kuboresha utendaji kazi. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla. Alikabidhi Magari hayo Oktoba 3, 2024 baada ya kufungua Mkutano wa Menejimenti ya WMA uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akikata utepe kabla ya kukabidhi magari kwa Wakala wa Vipimo (WMA) ili kusaidia kuboresha utendaji kazi. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla. Alikabidhi Magari hayo Oktoba 3, 2024 baada ya kufungua Mkutano wa Menejimenti ya WMA uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.

Ili kuhakikisha maono hayo ya Rais yanafikiwa, Dkt. Abdallah ameitaka WMA kuzingatia mambo kadhaa ambayo ni pamoja na utii wa sheria, miongozo na kanuni mbalimbali zilizopo kwa kuongeza uadilifu na weledi kazini.

Pia amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja na kuwa na kauli moja baina ya Bodi, Mkuu wa Wakala, Menejimenti, Viongozi wa Mikoa pamoja na wafanyakazi wote kwa lengo la kupata matokeo chanya katika kazi.

Vilevile ameielekeza Menejimenti kuondoa urasimu wa aina yoyote katika utendaji kazi huku akisisitiza kwamba Jarida alilozindua pamoja na kutoa habari mbalimbali za Wakala, litumike kama nyenzo ya utoaji taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na wadau wa WMA hususani katika ufanyaji biashara.

Katibu Mkuu amesisitiza Uongozi wa WMA kuzingatia yaliyomo katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja, ambao unaelekeza kutoa huduma bora na kwa wakati.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah (wa pili-kulia) akibadilishana mawazo na viongozi mbalimbali wa Wakala wa Vipimo (WMA) baada ya kufungua rasmi Mkutano wa Menejimenti ya Wakala uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, Oktoba 3, 2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua Mkutano wa Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) na kukabidhi magari kuboresha utendaji kazi, Oktoba 3, 2024 Kibaha mkoani Pwani.

Katika hatua nyingine, Dkt. Abdallah amempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa sekta mbalimbali za umma na kwa muktadha huo kwa WMA ambapo ametoa jumla ya magari 10 kwa Wakala hiyo ili kuboresha utendaji kazi.

“Leo nimekabidhi magari mawili kwa WMA na mengine Nane yako kwenye mchakato na tutayakabidhi mara moja utakapokamilika. Kwa hili, tuendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais,” amefafanua.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti nzima, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla amesema watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu.

Akidadavua kuhusu majukumu ya WMA ambayo ndiyo haswa yaliyotolewa maelekezo kuongeza nguvu, Kihulla amesema ni pamoja na uhakiki wa vipimo, ukaguzi wa vipimo pamoja na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa kwa lengo la kukuza uchumi katika sekta mbalimbali.

“Lengo ni kukuza uchumi katika sekta mbalimbali lakini pia kusaidia wananchi wanaonunua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na zinazotoka nje ya nchi, ziwe katika uzito sahihi, ujazo sahihi, urefu sahihi pamoja na namba yaani idadi sahihi.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla akizungumza na waandishi wa habari baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah kufungua Mkutano wa Menejimenti ya WMA na kukabidhi magari kuboresha utendaji kazi, Oktoba 3, 2024 Kibaha mkoani Pwani.

Kuhusu magari waliyopokea, Mtendaji Mkuu ameishukuru Wizara na kukiri kuwa yatapunguza changamoto iliyopo lakini akaomba Wakala iendelee kufikiriwa kupatiwa mengine zaidi pamoja na vitendea kazi vingine mbalimbali ili kuboresha zaidi utoaji huduma kwa wananchi.

Kikao hicho cha Menejimenti ya Wakala wa Vipimo ni utaratibu wa kawaida ambao Wakala umejiwekea ambapo hukutana kila robo ya Mwaka wa Fedha kujadili kuhusu maendeleo ya utendaji kazi na namna ya kuboresha zaidi. Kikao kiliketi kuanzia Oktoba 2, 2024 na kudumu kwa siku tatu ambapo kimejumuisha Menejimenti Kuu kutoka Makao Makuu pamoja na Mameneja wa Mikoa yote Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news