GEITA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka Watanzania kutunza sarafu kwa kuwa ni nyara ya Serikali na tunu ya taifa ambayo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha haiharibiwi.

“Serikali inatumia gharama kubwa sana kutengeneza na kuchapisha noti mpya kufidia zilizoharibika,” alisema Bi. Mosses.
Pia, amesema kuwa BoT imepokea taarifa za kuwepo kwa imani potofu katika baadhi ya maeneo ya uchimbaji madini, ambapo watu huchana noti kwa imani za kishirikina kama njia ya kuepuka ‘Chuma Ulete’.
Alisisitiza kuwa, kitendo hiki ni uharibifu wa fedha na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya kosa hilo kwa mujibu wa sheria.
“Kuna adhabu ya kifungo, faini, au vyote kwa pamoja kwa kosa hilo. Miezi michache iliyopita nilikuwa Mwanza, na tulishuhudia watu wakirusha pesa chini kwenye sherehe. Hii ni moja ya elimu tunayoitoa mara kwa mara kupitia Benki Kuu, ikiwataka watu kutumia vikapu maalum kwa ajili ya kutunza pesa,” alifafanua Bi. Mosses.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Mabenki kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Mamy Katikiro, alisema BoT inatambua changamoto zinazotokana na taasisi ndogo za fedha ambazo hazijasajiliwa, hasa zile zinazotoa mikopo mtandaoni.
“Kumekuwa na wimbi la taasisi zinazotoa mikopo mtandaoni ambazo hazijasajiliwa, na BoT imeendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa kukopa katika taasisi zilizosajiliwa na BoT,” alisema Bi. Katikiro.
Alibainisha kuwa BoT imeanzisha kampeni ya ZINDUKA USIUMIZWE: KOPA KWA MAENDELEO ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mikopo hiyo, ambayo imepewa majina kama “Kausha Damu” kutokana na masharti magumu yanayowaumiza wananchi.

Mkutano huo umefanyika katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZ Bombambili mkoani Geita mpaka tarehe 13 Oktoba 2024.