NA GODFREY NNKO
KONGAMANO la Nane la Mwaka la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Tanzania kwa mwaka 2024 (8th Annual Tanzania ICT Conference) limeanza katika Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Siku ya kwanza ya kongamano hilo Oktoba 13,2024 imeangazia Wanawake katika TEHAMA ambapo siku ya pili litaangazia Vijana katika TEHAMA.
Kongamano hili linatarajiwa kudumu hadi Oktoba 17, 2024 huku mgeni rasmi akitararajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb).
Pia, kupitia kongamano hilo, Tanzania ni mwenyeji wa kilele cha Shindano la Kwanza la Vijana la Afrika kwenye Masuala ya Akili Mnemba na Roboti (The African Youth in Artificial Intelligence and Robotics Competition).
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini (ICT Commission),Dkt.Nkundwe Mwasanga amesema, licha ya heshima hiyo kubwa ambayo Tanzania imepewa, pia ameendelea kuishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia.
Amesema,kwa upande wa mawasiliano nchini, kuna hatua kubwa imepigwa na nguvu zaidi inaendelea kuwekezwa huko ili kuhakikisha kila kona ya nchi inakuwa na mawasiliano ya uhakika.
"Tanzania ukiangalia soko lake la kidigitali ni kubwa mpaka sasa hivi namba za simu janja tulizonazo ni kama milioni 21. Kwa hiyo,ni namba kubwa sana hilo ni soko kwa maana yake.
"Sehemu ambayo una namba kubwa ya simu janja maana yake ukiandika programu yoyote ukapata watu laki moja kuna hela fulani utapata.
"Kwa hiyo Tanzania ukiangalia kwa mapana yake tunafanya vizuri sana katika mambo ya uchumi wa kidigitali."
Amesema, licha ya changamoto ziizopo kutokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia wanaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha mambo yanazidi kuwa mazuri zaidi.
"Teknolojia zinapokuja kitu cha kwanza unatakiwa uandae watu waanze kuitumia katika shughuli zao za kawaida.
"Kwa hiyo,suala la elimu ni suala ambalo halitaisha kila wakati tunatakiwa tutoe elimu zaidi ili kuwawezesha Watanzania wengi kuitumia teknolojia kama fursa.
"Sasa katika masuala ya elimu kuna mambo kama matatu. Kwanza kuna elimu ile ya kawaida ambayo inatakiwa Watanzania wote waipate ili waweze kuitumia Akili Mnemba katika shughuli zao za kawaida.
"Kuna elimu ya katikati ambayo wanaipata hawa mafundi wa ku-repair simu na mambo mengine.
"Halafu kuna elimu ya juu ambayo itawafanya watu sasa kuwa wabunifu. Ubunifu ndiyo unaofanya vitu viwili vikubwa katika uchumi wowote duniani.
"Kwanza ubunifu ndiyo unaotengeneza kazi, cha pili ubunifu ndiyo unaoifanya TEHAMA iweze kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi."
Pia amesema vituo vya ubunifu vitajengwa mikoa ya Lindi,Tanga,Arusha,Mwanza, Dodoma,Mbeya, Dar es Salaam na Zanzibar.
"Kwa hiyo ni vituo nane, lakini ndani ya vituo vya Arusha na Dar es Salaam kutakuwa na vituo vingine viwili vya kutengeneza vifaa.
"Kwa hiyo ukivihesabu vyote utakuta ni 10, kwa nini tumefanya hivyo? Tumefanya hivyo kwa sababu nchi yetu ina vijana wengi, wapo karibu milioni 21 wenye umri kati ya miaka 15 na 34.
"Hao wanaijua teknolojia na hao wana uwezo mkubwa wa kufanya ubunifu kwa sababu vijana ndiyo ambao wana uwezo mkubwa.
"Sasa, tumetengeneza hivyo vituo ili vijana wakiwa na ubunifu waweze kwenda pale kuanzisha kampuni zao.
"Wataweza kukaa pale kwa miezi kama 10 bure ili aweze kukuza kampuni halafu aweze kutoka.
"Lakini, sekta binafsi na wenyewe wana vituo mpaka sasa hivi ninavyojua vipo 52 vya taasisi mbalimbali za sekta binafsi.
"Ingawa ninajua changamoto ni kubwa kwa sababu vijana ni wengi, hivi vituo vinatakiwa viwepo kila wilaya ikiwezekana ambavyo vitasaidia TEHAMA isambae kote na TEHAMA iweze kuleta matokeo ambayo watu wanategemea kuyapata."
Amesema, Tume ya TEHAMA ambayo ni taasisi ya Serikali ina majukumu mawili ikiwemo kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA na mwisho ni kukuza TEHAMA hapa nchini.
Kwa upande wa kuratibu amesema kuwa, wamekuwa wakifanya kazi na taasisi zote za umma zikiwemo binafsi ili kuhakikisha kwamba, yale yaliyomo kwenye sera yanatekelezwa vizuri na kama kuna changamoto wahakikishe kwamba wanazitatua.
"Kwenye ukuzaji tunakuza wataalamu, tunakuza kampuni hizi ndogo (startups), tunakuza uchumi wa kidigitali kwenye mikoa yote Tanzania na vilevile ni kuifanya Tanzania iwe shindani katika uchumi wa kidigitali duniani."
Amesema, kwa upande wa tathimini ya usalama mtandaoni, Tanzania ipo katika kundi la kwanza Duniani ambapo wamefanya vizuri na kupewa alama 99.27.
"Kwa hiyo, hapo tumefanya vizuri, kuhusiana na kutoa huduma kwa wananchi, utoaji wa huduma sisi ni katiya nchi bora 25 na ukiangalia maeneo ya ujasiriamali ya vijana wa kidigitali watu wengi wamechukua hizo fursa hizo katika kutumia mitandao kuweza kufanya shughuli zao."
Vilevile kwa upande wa mawasiliano, amesema kuwa Mkongo wa Taifa umefikishwa katika wilaya nyingi nchini.
"Minara inajengwa ya kutosha na tuna project kubwa ya kufikisha mawasiliano sehemu ambazo hazijafikiwa na kampuni za simu na vilevile Tanzania ipo mbioni kurusha satelite yake."