Kujifungua salama ni haki ya msingi kwa kila mwanamke-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, kujifungua salama ni haki ya msingi kwa kila mwanamke hivyo Serikali inachukua hatua zote muhimu kuhakikisha haki hiyo inapatikana.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 4,2024 katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar wakati wa kilele cha hafla maalum ya shukrani ya kampeni ya “Uzazi ni Maisha” inayohusu kuchangia katika Mradi wa Upatikanaji wa Vifaa Tiba, ulioendeshwa na Taasisi ya Amref Tanzania.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kupitia mradi huo, Zanzibar imo katika njia sahihi ya kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, na ameipongeza Amref kwa mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana.

Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kampeni ya “Uzazi ni Maisha” imeongeza wigo mpana kwa akina mama kujifungua salama, na watoto kuwa katika mazingira na maisha bora baada ya kuzaliwa.
Vilevile Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wadau kuwa katika mwaka wa 2023 nchi imepata mafanikio makubwa kupitia upatikanaji wa vifaa tiba, kupitia Mradi wa Amref, kwa kufikisha huduma za matibabu katika maeneo ya mbali yenye shida ya matibabu.
Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau na sekta binafsi katika kuimarisha sekta ya afya, hususan afya ya mama na mtoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news