Kukosa misimamo kunatugharimu CHADEMA, kiukweli aibu naona mimi

MARA-Leo ni Oktoba 16,2024. Ni siku 45 zimesalia kabla ya sisi Watanzania kuingia vituoni kwa ajili ya kuchagua viongozi wetu wa Serikali za Mitaa wakiwa ni msingi muhimu wa maendeleo katika jamii zetu hapa nchini iwe mijini au vijini.

Tayari, kiongozi mwenye dhamana ambaye ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa alishatangaza rasmi tarehe ya uchaguzi huo ambao utafanyika Novemba 27,2024 hapa nchini.

Nikiwa hapa Tarime, mimi kama shabiki na mwanachama mwaminifu wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA) kwa zaidi ya miaka 20 sasa, nimegundua kuwa, misimamo ya viongozi wa chama chetu kuanzia ngazi ya Taifa hadi kanda,

Na wakati mwingine wale ambao wanatuunga mkono huenda ikatugharimu na tunaweza kupotea katika ramani ya kisiasa.
Miongoni mwa sababu za sisi kupotea katika ulingo wa kisiasa ni pamoja na vikauli kauli, maneno maneno au misimamo ya mara kwa mara ambayo haina kichwa wala mkia.

Si tu kwamba, misimamo hii imekuwa ikitufanya tuonekane kuwa wajinga bali inachangia hata sisi wenyewe miongoni mwetu kuonekana hatujitambui na hatujui kile ambacho tunakihitaji.

Katiba

Tukirejea katika misimamo hiyo, mathalani mwezi Mei, 2021 Mwenyekiti wa chama Taifa, Freeman Mbowe alisema kwa kinywa chake kuwa, bila Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya chama hakitashiriki uchaguzi.

Chairman Mbowe unaukumbuka msimamo huu au nikukumbushe,haya uliyanena wakati ukizungumza na Kamati ya Utendaji ya mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini. Miongoni mwa mikoa hiyo walikuwa wajumbe kutoka Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

"Ndugu zangu tunahitaji kufanya movement ya Katiba na Tume Huru ya Uchaguzi. Tumesema, hatutakwenda kwenye uchaguzi wowote na tume hii. Tunawafundisha makamanda wetu kuanzia ngazi ya chini kuhusu umuhimu wa katiba na ulazima wa katiba.

"Tutaitafuta, tutaipigania katiba ya nchi yetu kabla ya uchaguzi. Tunajipanga,"alisema Mbowe wakati huo.

Kigaila

Novemba, 2022 Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama,Benson Kigaila naye aitilia mkazo kuwa,Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hatutashiriki katika uchaguzi mkuu wa 2025 wala uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 iwapo hakutapatika Katiba mpya itakayoweka mifumo mizuri ya uchaguzi

"Chaguzi hizi ndogo hatutashiriki, uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, uchaguzi mkuu 2025, kama hakuna na katiba mpya itakayozaa Tume Huru ya Uchaguzi sheria bora za uchaguzi na mfumo bora wa tume kama hivyo vitu havipo uchaguzi huo hautafanyika sio kwamba hatutashiriki na wanaotaka kushiriki hawatashiriki."

Lissu

Vile vile Februari, 2023 Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu alikaririwa akisema kuwa,bila katiba mpya chama chao hakitashiriki uchaguzi mkuu wa 2025.

Lissu ambaye sisi makamanda tunamtania kama mzee wa matamko na misimamo iyokuwa na matokeo kwa kuwa mara zote kila mmoja anaangalia maslahi yake, alisema kuwa, yeye binafsi hatagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi ipatikane Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

"Kimsingi CHADEMA tutaonekana watu wa ajabu sana kama tutashiriki Uchaguzi mkuu wa 2025 kwa Katiba hii na Tume hii ya Uchaguzi,"alikaririwa Lissu.

Mnyika

Mbali na hayo, kwa nyakati tofauti mwaka 2023 na mwaka huu 2024, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika alikaririwa akisema kuwa,maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025 yanaendelea vizuri.

Ndani ya mwezi huu wa Oktoba, 2024 Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika akizungumza na wanahaari jijini Dar es Salaam alisema, ni muhimu kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari Oktoba 11 hadi 20 ili waitumie vizuri haki yao ya kuchagua viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji nchini.

“Nimewaita kupitia kwenu kuwatangazia Watanzania wote wenye sifa ya kupiga kura ambao ni wakazi wa mtaa wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, kuanzia Oktoba 11 mpaka 20, kote nchini wanapaswa mjitokeze kwenda kujiandikisha kwa wingi.

“Niwaambie Watanzania wote wafahamu kuwa na kadi ya mpigakura, kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura lililo chini ya Tume Huru ya Taifa Uchaguzi (INEC) hakutoi uhalali wa mwananchi kupiga kura kwenye uchaguzi wa vijiji na vitongoji kama jina lako halijaingia kwenye orodha ya wapigakura inayoandikwa hivi sasa,” alisema.

Mnyika alitoa rai kwa viongozi wa dini, asasi, taasisi za kiraia na vyombo vya habari kutumia wajibu wao kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha, ili wapate haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi kwenye uchaguzi huo.

Pia, alisema wanachama wa chama hicho kwa sasa wametawanyika sehemu mbalimbali wakihamasisha umma kujiandikisha, lakini jitihada za chama hicho peke yake hazitoshi kwa kuwa na wao pia wanajiandaa kwa kuweka wagombea katika uchaguzi huo.

Mbowe tena

Katika hatua nyingine mwezi Julai, 2024 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe akiwa katika mikutano ya Operesheni +255 Katiba Mpya katika Kanda ya Kaskazini alisema hawatasusia uchaguzi, badala yake watapambana kuwatoa waliopo madarakani.

Mikutano hiyo ilifanyika kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Nasai na Muriet jijini Arusha ambapo, wanachama wengi walishangazwa na msimamo huo ikiwa awali alitangaza chama hakitashiriki chaguzi zijazo.

"Tuishinda kwa tume iliyopo sasa na katiba hii hii, sasa kama hawatoi katiba mnataka tususe uchaguzi, au tupambane hivi hivi?. Hatuwezi kususa shamba la mahindi kwa nguruwe,tutawakabili wanavyokuja na tunawahakikishia tutashinda na tuna uwezo huo."

Mrema

Aidha, kupitia uchaguzi huo ambao awali walisema, hawatashiriki kupitia misimamo yao, Oktoba 15, 2024 katika makao makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam, mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema aliibua tuhuma mbalimbali kuhusu zoezi la uandikishaji wananchi katika daftari.

Miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na madai ya andikishaji wa watoto ambao hawajafikisha miaka 18 akimaanisha ni wanafuzi, pia waandikishaji kuruka namba kwenye dafttari la uandikishaji huku wakiwa na waangalizi wao.

Vilevile,madai ya uwepo wa vituo nyumbani kwa viongozi na majengo ya chama tawala huku akijua kuwa, anayoyasema hayasadifu ukweli wowote kwa kuwa mambo kama hayo hayapo.

Kwa mwenendo huu, nikiri wazi kuwa sisi CHADEMA hatujielewi na wenzetu hawatueleweki. Kwa miaka mitatu tumekua tukisema hatutashiriki uchaguzi wowote bila katiba mpya. Hivyo, ikaonekana wazi kuwa tuliweka mayai yetu yote kwenye kapu la katiba mpya bila kujiandaa na chaguzi.

Leo tumebadili gia angani,tumekubali kushiriki chaguzi bila maandalizi yoyote na hata kabla ya mapambano tumeanza visingizio. Kwa kweli ndugu zangu wana CHADEMA aibu Naona Mimi.

Tunatoa visingizio kwa sababu tunajua hatujajiandaa na chaguzi za serikali za mitaa ni rasharasha tu, je uchaguzi mkuu itakuwaje. Kiuweli Aibu Naona Mimi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news