Lengo ni kuifanya Zanzibar kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na kupokea meli kubwa-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, mapinduzi makubwa katika sekta ya miundombinu ya bandari yanalenga kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha usafirishaji na kupokea meli kubwa zinazoleta bidhaa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Zanzibar Multipurpose Terminal. Nicolas Escalin (kulia kwa Rais) na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Mhe.Dkt.Khalid Salum Mohammed wakati akitembelea Bandari Kavu Maruhubi Wilaya ya Mjini Unguja, baada ya kuifungua na kushoto kwa Rais ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa tamko hilo leo Oktoba 18,2024 alipoifungua Bandari kavu ya Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kuwa, ufunguzi wa Bandari kavu ni hatua muhimu ya kuimarisha utendaji wa bandari kwani itapunguza msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza, mabadiliko hayo ya Miundombinu ya Bandari yataleta msukumo mkubwa wa ukuaji wa Uchumi wa Zanzibar na kuwasisitiza wadau kuunga mkono juhudi hizo.

Ameeleza kuwa kampuni ya Africa Global Logistic inayoendesha bandari ya Malindi hivi sasa inaendelea kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji yanayoongeza Ufanisi na kuwapa urahisi Wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao bila usumbufu pamoja na kuokoa muda.

Dkt. Mwinyi amewahakikishia wadau kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kufanya kazi zaidi na sekta binafsi kwani mbali ya kuja na mitaji, pia wanakuja na utaalamu na teknolojia za kisiasa zinazochochea ufanisi kwenye utendaji.


Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali ianendelea na Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani kwa kuifanya kuwa yenye uwezo wa kuhudumia meli nyingi zaidi ikwemo kampuni za kimataifa kuleta meli za mafuta kwenye bandari hiyo.

Amesisitiza, bado kuna fursa zaidi za kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa bandari zote na kuziagiza taasisi za TRA, ZBS, ZFDA, taasisi ya Atomic energy, na Mkemia Mkuu wa Serikali kuongeza kasi na ufanisi katika utendaji wao ili kuwarahisishia Wafanyabiashara mazingira bora ya ufanyaji wa biashara yatakayopunguza gharama na kumpa unafuu mtumiaji.

Amebainisha kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi imedhamiria kuendesha huduma za bandari kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia bandari ni lango kuu la uchumi kwa nchi.

Aidha, amesema Serikali kupitia mradi huo utawapunguzia gharama kubwa wafanyabiashara.

Ameeleza hatua hiyo pia itasaidia harakati za uendeshaji kuwa zenye ufanisi, kuongeza tija na kupunguza gharama za uletaji mizigo (freight price) ndani ya nchi.

Pia Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wafanyabiasha kuwa Serikali inaendelea kuwawekea mazingira rafiki hasa kwa ujenzi wa miundombinu.

Alisema, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali ili kuendeleza sekta ya Uchukuzi na kuimarisha jitihada za pamoja za kuleta mafanikio ya kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege Unguja na Pemba ili kuwarahisishia huduma wananchi na wageni wanaoitembelea Zanzibar.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesihi wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa kuwazingatia wananchi hasa kuwapunguzia makali ya bei za bidhaa kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza gharama za usafiri.

Waziri wa Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Muhammed amesema, mageuzi na mafanikio yaliyofikiwa kuimarisha sekta ya Bandari ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025.

Aidha, amesisitiza kuwa mabadiliko yanayoendelea kwa kuziimarisha Bandari yanaenda kuifanya Zanzibar kufikia malengo na matarajio ya kuhudumia Meli takriban laki tatu kwa mwaka.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Atif Khamis ameeleza dhana ya ushirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi imekuwa kuchochea mabadiliko makubwa ya utendaji wa shirika la Bandari na kuelezea ufunguzi wa Bandari kavu utaongeza mapato ya shirika na kupunguza msongamano wa makontena Bandari ya Malindi.

Pia,amesema kuna ongezeko la mapato kwa asilimia 15 tangu kampuni binafsi kuingia ushirikiano na Serikali kuiendesha Bandari ya Malindi, kupungua kwa muda wa Meli kusubiri gati kwa asilimia 75 na muda wa kutoa Makontena kutoka siku 40 hadi siku 7 hadi kumi hivi sasa kwa asilimia 50.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news