NA MARY GWERA
Mahakama Zimbabwe
MAHAKAMA za Katiba barani Afrika zinao wajibu wa kuhakikisha kuwa, zinakuza na kuhifadhi utu na haki za msingi za binadamu ili kuleta ustawi wa haki za Waafrika na Dunia kwa ujumla.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) pamoja na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman (kulia) wakiwa katika Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) ulioanza kufanyika leo tarehe 31 Oktoba, 2024 mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Hayo yamesemwa leo tarehe 31 Oktoba, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Jenerali Mstaafu Mhe. Dkt. Constantino Chiwenga wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) unaofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe ambao umehudhuriwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Majaji Wakuu wengine na Wadau wa Sheria kutoka nchi mbalimbali.
“Heshima ya utu wa binadamu ipo katika Katiba ya nchi karibu zote, hivyo ni wajibu wetu kusimamia na kulinda, kuheshimu haki na utu wa binadamu,” amesema Mhe. Dkt. Chiwenga.
Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Jenerali Mstaafu Mhe. Dkt. C.G.D.N Chiwenga akifungua Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA) leo tarehe 31 Oktoba, 2024 unaofanyika mjini katika Hoteli ya 'Elephant' mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Makamu huyo wa Rais ambaye amemwakilisha Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa amesema kuwa, anategemea kwamba kupitia Mkutano huo wataalamu wa Sekta ya Sheria watatoka na njia za kifanisi zaidi zitakazotumiwa na Mahakama kuangalia haki za msingi za kibinadamu.
Aidha, ameongeza kuwa, mbali na Mahakama hizo, Mihimili mingine ya Dola kwa maana ya Serikali na Bunge inayo pia wajibu wa kutekeleza na kusimamia utu na haki za binadamu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifuatilia kinachojiri katika mkutano huo. Kulia ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimuonesha kitu Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa saba ya Mahakama za Mamlaka ya kikatiba Afrika (CJCA) unaofanyika mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) unaofanyika Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Rais wa Mahakama ya Katiba ya Ufalme wa Morocco ambaye pia ni Rais wa Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA), Mhe. Mohammed Amine Benabdallah akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) leo tarehe 31 Oktoba, 2024 mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi, naye Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Zimbabwe, Mhe. Luke Malaba amesema, ni muhimu Mahakama za Kikatiba kushirikiana kwa karibu ili kuendelea kulinda utu na haki za binadamu.
“Binadamu wote tumezaliwa tukiwa huru na sawa, hivyo ni vema Mahakama kulinda utu na haki na uhuru wa binadamu wote kwa usawa,” amesema Mhe. Malaba.
Amesema, Mahakama za Kikatiba zinazo mamlaka ya kusimamia haki na utu wa binadamu na kwamba kupitia Mkutano huo ni vema kuangalia njia bora zaidi za kuulinda utu wa binadamu kwa heshima.
Naye, Rais wa Mahakama ya Katiba ya Ufalme wa Morocco ambaye pia ni Rais wa Mamlaka ya Kikatiba ya Afrika (CJCA), Mhe. Mohammed Amine Benabdallah, amesema kuwa, watahakikisha wanashirikiana na Nchi mbalimbali kusimamia na kulinda haki na utu wa binadamu.
Sehemu ya Maafisa wa waliombatana na Jaji Mkuu wa Tanzania wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA) unaofanyika katika Hoteli ya Elephant mjini Victoria Falls nchini Zimbabwe.
“Haki za binadamu ni suala muhimu sana na hivyo ni muhimu kuzihifadhi, hivyo ushirikiano ni kitu muhimu katika utekelezaji wa suala hili,” amesema Mhe. Benabdallah.
Ameeleza kwamba, Kongamano hilo litasaidia kupata muda wa kujadili malengo waliyojiwekea na hatimaye kuwa na mtazamo wa pamoja kuhusu umuhimu wa kusimamia na kulinda utu wa kibinadamu.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo; Utu wa binadamu kama thamani ya msingi na kanuni: Chanzo cha tafsiri ya kikatiba, ulinzi wa haki za msingi za binadamu na utekelezaji.
Picha mbalimbali za washiriki pamoja na waalikwa wakifuatilia kinachojiri katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo.
Meza kuu ikiongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Jenerali Mstaafu Mhe. Dkt. Constantino Chiwenga (katikati) katika picha ya pamoja na sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Saba wa Mahakama za Mamlaka ya Kikatiba Afrika (CJCA).(Picha na MARY GWERA, Mahakama ya Tanzania).
Katika mkutano huo, washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu na kufahamu kuhusu Katiba na Sheria za Nchi zao zinasemaje kuhusu haki na utu wa binadamu.
Mahakama ya Tanzania ni moja wa Washiriki wa Mkutano huo muhimu, nchi nyingine zinazoshiriki Mkutano huo ni Zambia, Malawi, Msumbiji, Lesotho, Afrika Kusini, Namibia, Somalia, Sierra Leone, Togo, Uturuki, Misri, Ushelisheli, Urusi, Senegal na nyingine.