Majaji wa Rufani mna mchango uboreshaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi-Jaji Mkuu Prof.Juma

NA MARY GWERA
Mahakama Arusha

MAHAKAMA ya Rufani Tanzania inayo nafasi ya kuboresha Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kupitia Rufaa zinazokatwa na wafanyakazi ambao hawakuridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu yanayohusu fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kupata magonjwa wakiwa kazini.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma akifungua kikao kazi kati ya Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha leo tarehe 07 Oktoba, 2024.

Hayo yamesemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 07 Oktoba, 2024 katika Hoteli ya ‘Mount’ Meru jijini Arusha wakati akifungua Kikao Kazi kati ya Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

“Utaratibu huu unatoa nafasi ya Mahakama ya Rufani katika nafasi yake ya mwisho ya kutafsiri Sheria, kuweka mizani sawa baina ya wanufaika wa Mfuko na uwezo wa Mfuko kuhimili madai ya malipo ya fidia,” amesema Mhe.Prof. Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma akifungua kikao kazi kati ya Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha leo tarehe 07 Oktoba, 2024.

Jaji Mkuu amesema Kikao kazi hicho baina ya Viongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Majaji wa Mahakama ya Rufani ni nafasi muhimu ya kutafakari nafasi ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 kwa kuwa Sera hiyo inajumuisha maeneo mengi yanayowagusa Watanzania ambayo yanahitaji hifadhi ya jamii.

“Hivyo, leo ni nafasi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa mfuko kuhusu Mfuko na nafasi ya Mahakama kama mtetezi wa haki kwa watu wote, napenda kuwasihi washiriki wote kuchangia kwa ufanisi. Mimi naamini majadiliano yoyote huzaa maboresho na mabadiliko,” ameeleza Mhe.Prof. Juma.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani wakisikiliza hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) leo tarehe 07 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya 'Mount' Meru.

Ameongeza kuwa, kikao hicho ni fursa kwa Mahakama ya Rufani kukaa pamoja na WCF ili kubadilishana mawazo, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho kwa masuala ya kikazi yanayohusiana na fidia kwa wafanyakazi au wategemezi wa wafanyakazi walioumia au kufa kutokana na kuumia kazini.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inatambua Umuhimu wa Hifadhi ya Jamii ambapo ametoa mifano kadhaa kuwa, Sehemu ya Pili ya Katiba, Ibara ya 8(1) (b) inasema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na Haki ya Jamii, kwa hiyo, Lengo kuu la Serikali litakuwa ni Ustawi wa Jamii.

“Maudhui ya Katiba ya Tanzania (1977) inaonesha Katiba kuipa hifadhi ya jamii nafasi kubwa katika ujenzi wa nchi inayozingatia uhuru, haki, udugu na amani,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu amempongeza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina kutekeleza kwa vitendo, Nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama kwa namna anavyoshirikiana na Mdau Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kutoa mafunzo kwa Majaji wa Mahakama Kuu na Majaji wa Mahakama ya Rufani.
Picha za juu ni sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Naibu Wasajili na Wadau kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na wengine wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).

“Kufanyika kwa vikao hivi ni ishara ya mafanikio ya ushirikiano baina ya Mahakama, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na wadau katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025 hususani nguzo ya tatu katika ushirikishwaji wa wadau katika utoaji haki kwa wakati,” ameeleza Mhe. Prof. Juma.

Ameongeza kwa kuipongeza Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa kuendeleza matumizi ya Majadiliano na Usuluhishi katika kutatua migogoro katika maeneo ya kazi na kwamba Mahakama hiyo imetekeleza matakwa ya Sheria kwa kushirikiana kwa ukaribu na Serikali, Vyama vya Waajiri, vyama vya Wafanyakazi, Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Mifuko ya Ustawi wa Jamii.

Akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina amesema, kikao hicho ni muendelezo wa vikao kazi ambavyo vimefanyika nchi nzima katika maeneo mbalimbali ikiwemo Bagamoyo, Mwanza, Arusha, Songea, Kigoma na Zanzibar ambavyo vilishirikisha Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili, Watendaji, Makamishna wa Kazi (Bara na Visiwani), Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), DHU, Watendaji pamoja na Watumishi wengine.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa kikao kazi kati ya Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha leo tarehe 07 Oktoba, 2024.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha leo tarehe 07 Oktoba, 2024. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma na wa kwanza kulia ni Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa.

“Mpaka sasa jumla ya Watumishi 311 wakiwemo Majaji wa Mahakama Kuu, Majaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Naibu Wasajili, Watendaji, Wadau na Watumishi wengine wamehudhuria vikao hivi,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.

Jaji Mfawidhi huyo amesema, sababu za kushirikisha Wadau ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/2021-2024/2025 hususani nguzo ya pili na ya tatu inayohusu kurejesha Imani ya wananchi kwa kutatua migogoro kwa wakati kwa kushirikisha Wadau.

Amesema ushiriki wa Mahakama ya Rufani ni muhimu, huku akirejea Kifungu 58 cha Sheria ya Taasisi za Kazi (Labour Institution Act) kinaweka bayana kuwa, pale ambapo kuna maamuzi yanayokinzana ya Mahakama Kuu, anawasilisha maombi ya Marejeo ‘reference’ Mahakama ya Rufani.

“Kanuni 53 Mahakama ya Kazi (Labour Court Rules) inaelekeza mahitaji ya hati ya uwepo wa hoja za kisheria kutolewa kwa Kamishna wa kazi anapotaka kufanya marejeo kwenda Mahakama ya Rufani,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati). Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Claud Mugeta, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa WCF, Dkt. John Mduma na wa kwanza kulia ni Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa WCF, Dkt. John Mduma leo tarehe 07 Oktoba, 2024 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kati ya Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika Hoteli ya 'Mount' Meru jijini Arusha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema, kama ilivyo kwa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mahakama ya Rufani Tanzania ni mdau muhimu katika Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kwa kuwa ndio Mamlaka ya juu ya Rufaa baada mfanyakazi anayedai fidia kutoridhika na uamuzi wa rufaa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya kazi na Mahakama Kuu – Divisheni ya Kazi.

“Kwa mantiki hiyo na hasa kutokana na jukumu hilo la Majaji wa Mahakama ya Rufaa katika utoaji wa uamuzi ya juu kabisa kwenye masuala yanayohusiana na madai ya fidia kwa wafanyakazi, kila mmoja atakubaliana nami juu ya umuhimu wa kikao kazi hiki. Tunaamini mwisho wa kikao hiki washiriki hawa watakuwa wamejifunza au kuongeza uelewa zaidi juu ya masuala kadhaa ya fidia kwa mfanyakazi,” amesema Dkt. Mduma.

Mbali na Kikao kazi hicho kilichowahusisha Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi huyo amesema kuwa, WCF imeshiriki pia kuratibu vikao kazi kama hivyo kwa watendaji wa ngazi mbalimbali za Mahakama ya Tanzania na kwamba Mfuko huo na Serikali kwa ujumla imefaidika na michango na mawazo mbalimbali yaliyokuwa yakiibuliwa na washiriki wa vikaokazi hivyo.
Meza kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili wa Mahakama na Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na Wawezeshaji.(PICHA NA MARY GWERA, Mahakama).

Amesema, michango hiyo imechangia kufanyika kwa maboresho au marekebisho kadhaa katika Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi na kwamba ana imani pia michango ya washiriki wa kikao kazi hicho itasaidia kuboresha zaidi tasnia hii ya fidia kwa wafanyakazi hapa nchini.

Katika kikao hicho cha siku mbili, mada mbalimbali zitatolewa ambazo ni pamoja na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263), Taratibu za Madai, Mikataba ya Kimataifa kuhusiana na Masuala ya kazi na matumizi yake nchini Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news