NA EUNICE LUGIANA
Mahakama Pwani
HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi ameweka bayana kuwa mashahidi ni moja ya kikwazo kinachosababisha ucheleweshaji wa mashauri na kutokufikia malengo ya kumaliza mashauri kwa wakati.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Haki Jinai baada ya kuzungumza na wafungwa na mahabusu katika Gereza la Mkuza mkoani Pwani.
Akizungumza katika Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika hivi karibuni katika Mahakama hiyo, Mhe. Mkhoi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikao hicho alisema, “licha ya kwamba mashahidi wanafika lakini sio kwa kasi ambayo tulikubaliana, hali hii inakwamisha maazimio tuliyojiwekea ya kuleta mashahidi kwa wakati ili kumaliza mashauri kama tulivyokubaliana ili kukidhi maazimio ya kikao kilichopita.”
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na Mwenyekiti wa Kikao cha Kusukuma Mashauri cha Mkoa huo, Mhe. Joyce Mkhoi akiwa katika kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni Katibu wa kikao hicho, Wakili wa Serikali Mwandamizi.
Alisema, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani imebaini sababu mojawapo ya ucheleweshwaji wa kumalizika kwa mashauri kwa wakati kuwa ni pamoja na mashahidi kutokufika mahakamani hasa Polisi, ambapo kumekuwa na sababu mbalimbali ikiwepo ya kuwa masomoni na kuwa katika kazi nyingine.
Aidha, Mfawidhi huyo aliwaomba Polisi pamoja na Mawakili wa Serikali kujitahidi kuleta mashahidi kwa wakati ili kumaliza mashauri na kuepuka mlundikano wa mashauri.
Naye, Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Salum Ally alisema mashahidi wamekuwa na utaratibu wa kufika mahakamani kwa kuchelewa au kutofika kabisa hivyo, Mahakama kuchelewa kuanza kwa wakati uliopangwa.
Akitoa mfano, Mhe. Ally alisema, “kuchelewa kufika mahakamani kwa mashahidi kunasababisha kuchelewa kuanza kwa Mahakama na hivyo kusikiliza mashauri mpaka jioni hii inasababisha mashahidi kutosikilizwa wote na hivyo kupangiwa tarehe nyingine.”
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani , Mhe. Salum Ally akichangia jambo wakati wa kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni.Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Wilaya ya Kisarawe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Joseph Matui alisema lawama nyingi ziko kwa Polisi kwakuwa wako na majukumu mengi ya kukamata watuhumiwa, kufanya upelelezi na kwamba unapofika wakati wa kutoa ushahidi wanakuwa wamepangiwa jukumu jingine ambapo aliweka bayana kuwa ndipo changamoto inapoanzia.
Mrakibu Matui aliwataka wadau wa haki jinai kuelewa kuwa Polisi wa majukumu mengi wanapotoa udhuru wa kutoa ushahidi kwa wakati huo, waelewe kuwa kuna majukumu mengine.
Katika kikao hicho, wajumbe waliazimia kuwa, kufikia tarehe 15 Desemba mwaka huu mashauri yaliyobaki katika Mahakama hiyo yawe yamemalizika.
Kabla ya kikao hicho kuanza, kilitanguliwa na ziara ya ukaguzi wa Gereza la Mahabusu Mkuza ambapo Wadau wa Haki Jinai walifika gerezani hapo na kuzungumza na wafungwa na mahabusu, kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili mahabusu na wafungwa hao ambapo kero nyingi zilitatuliwa kwa asilimia kubwa.
Wakati huohuo, Afisa kutoka Ofisi ya Huduma kwa Jamii (adhabu mbadala ), Bw. Deogratius Njuu ametoa taarifa ya wafungwa wa nje kuwa, watakuwa wanafanya kazi za usafi kwenye Ofisi za wadau wa haki jinai kwa mwezi mara moja.
Kwa mujibu wa Bw. Njuu amesema utaratibu huo ulikuwa ukitumika kipindi cha nyuma na sasa wameona ni vema kuurejesha tena.
Aliwaomba wadau hao kuhakikisha vitendea kazi vinakuwepo na kazi inafanyika ndani ya saa nne kwa siku na si zaidi ya hapo.
Wafungwa na mahabusu hao waliushukuru uongozi wa Mahakama na kuomba mashauri ambayo hayana dhamana waweze kupatiwa dhamana, ambapo katika hilo, Mhe. Mkhoi alisema Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria na sio kutunga sheria, hivyo Mahakama inafanya kazi yake na sio kazi ya chombo kingine.
Afisa Huduma kwa Jamii, Bw. Deogratius Njuu akitoa maelezo kuhusu wafungwa wa kifungo cha nje kufanya usafi katika ofisi za wadau wa Haki Jinai.
Kikao cha Kusukuma Mashauri hufanyika mara tatu kwa mwaka na pia wadau wa haki jinai huweka maazimo na baada ya miezi mitatu hurudi na kuona kama maazimio yaliyowekwa yametekelezeka.
Maazimio mojawapo ya kikao kilichopita ni pamoja na kumaliza mashauri ndani ya miezi mitatu na mashauri sita kati ya kumi yaliyokuwa ya mrundikano yamemalizika.