Mavazi yanatuvuruga

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, kila mmoja wetu anatambua wazi kuwa,mavazi kwa maana ya nguo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa jamii mbalimbali duniani.
Aidha, licha ya kuwa sehemu ya urembo,pia mavazi huvaliwa kulingana na matukio, hafla au shughuli husika katika jamii.

Vilevile,wanaume huvaa mavazi tofauti na wanawake. Pia, mavazi ya watu wazima hutofautiana kidogo na mavazi ya vijana.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, licha ya umuhimu wa mavazi kwa kila binadamu, nyakati za sasa mavazi yanavuruga wengi kutokana na mitindo
yenye utata hasa kwa Waskochi. Endelea;

1.Mavazi yatuvuruga, hadi tunavurugika,
Kwa kweli yanaturoga, hadi watu twarogeka,
Yamekuwa ndiyo soga, hata Neno laachika,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

2.Je Mungu pale Edeni, mavazi yalihusika?
Adamu bustanini, suruali lijivika?
Eva livaa gauni, ubishi unatushika?
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

3.Ni Neno linahusika, mavazi yakagawika,
Au sisi twahusika, kwetu kutamadunika?
Hii ikieleweka, ubishi hatutashika,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

4.Pensi nyanya yahusika, Adamu aweze daka?
Vipi sketi kushika, Waskochi waehuka?
Ni mila zinahusika, au ni wetu Rabuka?
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

5.Mungu wa ajabu sana, maishani ahusika,
Kama kimshika sana, takujuza ya kushika,
Mengine muhimu sana, mengine ni takataka,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

6.Kile kinaeleweka, Biblia ukishika,
Mavazi yanatajika, bila kufafanulika,
Na wale wanahusika, mila zaidi zashika,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

7.Muhimu mtu kushika, lengo likaeleweka,
Mila hasa zahusika, mavazi ya kutumika,
Neno la Mungu kishika, Edeni kunahusika,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

8.Kujisetiri kuzuri, macho yanaburudika,
Kuvaa hovyo kiburi, hilo linaeleweka,
Ila nguo zote nzuri, kwa jinsi zinavalika,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

9.Suruali kivalika, maridadi waoneka,
Jinsia zote husika, hiyo inakamilika,
Sawa kikoi hakika, jinsia zote chashika,
Bora tukajiuliza,majibu yakaonesha.

10.Mwisho kwao wenye chongo, kiingia wahusika,
Nawe jicho liwe fyongo, hapo utakubalika,
Ukileta longolongo, hupati unachotaka,
Bora tukajiuliza, majibu yakaonesha.

11.Mungu tupe maarifa, Neno tuweze kushika,
Tusilifanye ni dhifa, mila zetu kuchomeka,
Libaki na yake sifa, na sote tukilishika,
Bora tukajiuliza,majibu yakaonesha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news