Mazoezi ya kuondoa noti kwenye mzunguko ni kazi ya kawaida inayofanyika ulimwenguni kote-BoT

DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imekutana na waandishi wa habari nchini kufafanua kuhusu taarifa iliyotolewa hivi karibuni inayohusu zoezi la kuondoa noti za zamani kwenye mzunguko.
Noti hizi ni za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003.

Sambamba na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010 zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11 Oktoba 2024.

Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu, Bw. Ilulu S. Ilulu amesema, Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inaipa mamlaka BoT kuchapisha, kutangaza na kusambaza noti nchini.
“Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, sura ya 197, kifungu cha 26, kimeipa Benki Kuu mamlaka ya kuchapisha noti na kuzisambaza nchini Tanzania.

"Kifungu cha 27 (2), kimeipa mamlaka BoT kuzitangaza noti ambazo itakuwa imezichapisha ikiwemo kutoa tangazo katika Gazeti la Serikali kabla ya noti hizo kuingizwa kwenye mzunguko kwa ajili ya matumizi,” amesema Bw. Ilulu.

Ameongeza kuwa, Sheria hiyo inailekeza BoT kutoa muda wa kurejesha noti zilizoainishwa kwa ajili ya ukusanyaji wa noti hizo pamoja na kuziondolea uhalali wa kutumika.
"Pia, kifungu cha 28 (2) kinaelezea kwamba Benki Kuu itatoa muda kwa wananchi kurejesha noti zilizokusudiwa kwa ajili ya ukusanyaji.

"Hivyo zoezi hili litafanyika kupitia ofisi za Benki Kuu na benki zote za biashara. Aidha, kifungu cha 28 (3) cha sheria hiyo inaipa mamlaka Benki Kuu kusitisha uhalali wa fedha itakazoziainisha kadri itakavyoona inafaa kwa kuchapisha tangazo katika Gazeti la Serikali,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani siyo geni nchini na lilifanyika mara ya kwanza mwaka 1977.

“Tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu mwaka 1966, mazoezi ya kuondoa noti kwenye mzunguko yamefanyika mwaka 1977, 1979, 1980 na 1995.

"Kwa hiyo, kama tulivyoeleza, hii ni kazi ya kawaida ya Benki Kuu hapa nchini na ulimwenguni kote.”
Zoezi hilo linatarajia kuanza Januari 6, 2025 hadi Aprili 5, 2025, kupitia ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news