Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) wawezesha wananchi milioni 5.3 kupata maji ndani ya miaka mitatu

NA GODFREY NNKO

MFUKO wa Taifa wa Maji (NWF) umesema, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2024, miradi ya maji 354 kati ya miradi 998 iliyopokea fedha kutoka mfuko huo imekamilika na kunufaisha wananchi wapatao milioni 5.3.
"Hii ni kazi kubwa, na tutahakikisha fedha zinazokuja kwenye taasisi yetu tunaendelea kuzitoa na kuzielekeza maeneo husika ili wananchi waweze kupata huduma bora za maji nchini."

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF),Wakili Haji Nandule ameyasema hayo leo Oktoba 31,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

NWF ambao unasimamiwa na Wizara ya Maji pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yapo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema,Mfuko wa Taifa wa Maji umeanzishwa chini ya Sheria ya Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 05 ya Mwaka 2019.

"Hii ni taasisi ya fedha yenye lengo la kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya usambazaji majisafi kwenye maeneo yenye uhaba na utunzaji wa vyanzo vya maji nchini."

Wakili Nandule amesema,uanzishwaji wa mfuko unalenga kuwa na uwepo wa chanzo cha fedha cha uhakika cha kutekeleza miradi ya maji.

"Kwa hiyo,kubwa ni kukamilika kwa miradi 354 katika kipindi hicho na hadi kufikia Julai 2024, jumla ya shilingi bilioni 5.3 zimetolewa kama mikopo kwa mamlaka za maji,"amesisitiza Wakili Nandule.

Pia, amesema takribani miradi 104 ya uhifadhi na uendelezaji wa vyanzo vya maji imetekelezwa nchini.

Wakili Nandule amesema, miradi hiyo inajumuisha uhifadhi wa vyanzo vya maji zaidi ya 92 ikiwemo chemichemi, vidakio vya maji, maziwa,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho.

Mabwawa, mito na visima ikiwemo ujenzi wa bwawa moja na ukarabati wa mabwawa saba, uchimbaji wa visima virefu zaidi ya 50 pamoja na kurudisha mito mitano iliyopoteza mikondo yake.

Wakili Nandule ameongeza kuwa, wapokeaji wa fedha za miradi ya mfuko ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), mamlaka za maji na bodi za maji za mabonde.

Mfuko wa Taifa wa Maji unatekeleza majukumu yake chini ya Sheria ya Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019.

Huduma zinazotolewa na mfuko zinatokana na majukumu yaliyoainishwa kwenye Sheria katika Kifungu cha 56 ((a) – (g)) kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kusaidia uwekezaji kwenye miradi ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Vilevile,kutuma fedha kwa watekelezaji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji, kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa watekelezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye miradi ya maji.

Jukumu lingine ni kufuatilia matumizi ya fedha zinazotumwa kwa watekelezaji, kujengea uwezo watekelezaji wa miradi ya maji ili waweze kusimamia kwa ufanisi miradi inayotekelezwa.
Aidha,mfuko una jukumu la kumshauri Waziri wa Maji kuhusu miongozo ya utoaji mikopo kwa mamlaka za maji.

Sambamba na kuandaa miongozo ya kiutendaji kuhusu utoaji wa mikopo na misaada kwa matekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Wakati huo huo, Wakili Nandule amesema, kwa sasa chanzo kikubwa cha fedha kwa mfuko huo ni tozo ya mafuta ya shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ya Petroli na Dizeli. 

"Tozo hii inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha Namba 16 ya Mwaka 2015,"amesisitiza Wakili Nandule ambapo mfuko huo umekuwa ukitoa ruzuku na mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na uhifadhi vyanzo vya maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news