GABORONE-Mkuu wa Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (𝗦𝗔𝗗𝗖-SEOM), Mhe. Mizengo Pinda amefunga mafunzo maalum yaliyoendeshwa na Secretariet ya SADC kwa waangalizi wa misheni hiyo wanaotoka katika nchi wanachama wa SADC.


Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Mhe. Pinda amewasihi waangalizi hao kuhakikisha wanazingatia misingi na miongozo yote waliyopatiwa wakati wa mafunzo na hivyo kutekeleza jukumu la uangalizi kwa mafanikio.
“Mmekuwa hapa kwa muda wa siku nne, ni matumaini yangu kuwa mmeelewa na mtazingatia mafunzo mliopewa, niwasihi muhakikishe mnafuata na kuzingatia misingi na miongozo mliyopewa na waendesha mafunzo, mjue kuwa sasa kazi imeanza na kilichobaki ni kutekeleza jukumu la uangalizi ambalo lipo mbele yetu,” alisema Mhe. Pinda.

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Sekretarieti ya SADC na Taasisi ya Uchaguzi kwa Demokrasia Endelevu Afrika (EISA), yaliangazia masuala mbalimbali ya kisera na kisheria ya Botswana, kikanda na kimataifa ambayo hutumika kusimamia uchaguzi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha demokrasia na utawala bora katika ukanda wa SADC.

Katika Uchaguzi mkuu huo wananchi wa Botswana watachagua Wabunge wa Bunge la 13 la nchi hiyo na wajumbe wa Mabaraza ya Mitaa ambapo viti 61 vya Bunge la Taifa na viti 609 vya mabaraza ya mitaa vitashindaniwa. SEOM inatarajiwa kupeleka waangalizi wa uchaguzi katika wilaya, miji na majiji yote nchini Botswana.