GABORONE-Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM),Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na kuzungumza na Wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao nchini Botswana katika kikao kilichofanyika jijini Gaborone tarehe 26 Oktoba 2024.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Pinda amewaelezea wanadiplomasia hao kuwa SEOM ina jukumu la kuangalia Uchaguzi Mkuu wa Botswana kama unaendeshwa na kuzingatia misingi na miongozo iliyowekwa na SADC kwa lengo la kukuza na kulinda kidemokrasia kwenye ukanda wa SADC.
Ameeleza kuwa SEOM imekutana na wadau mbalimbali ikiwa ni sehemu ya majukumu ya misheni hiyo ya kukutana na kuzungumza moja kwa moja na wadau mbalimbali wa uchaguzi huo ili kupata picha halisi ya jinsi mwenendo na maandalizi ya uchaguzi huo unavyokwenda.
Amesema SEOM imekuwa ikiangalia jinsi mwenendo, mipango na utaratibu wa uchaguzi huo unavyoendeshwa kwa, kuangalia kama elimu kwa wapiga kura imetolewa vya kutosha, kama inaendelea kutolewa kwa wadau wote wa uchaguzi huo na kama kumekuwa na ushirikishwaji kwa wadau wote wa uchaguzi nchini humo na hivyo kuwa na uelewa wa pamoja kuhusiana na uchaguzi mkuu huo uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba,2024.
Amesema SEOM imepeleka waangalizi wake katika majimbo yote ya uchaguzi ili kuangalia hali inavyokwenda, itakavyokuwa siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na wataendelea kukutana.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mabalozi hao na Balozi wa Jamhuri ya Angola Mheshimiwa Beatriz Morais ameishukuru SEOM kwa kukutana na mabalozi kama moja ya wadau wa uchaguzi wa Botswana ili kusikiliza mtazamo wao kuhusiana na mwenendo wa uchaguzi na kuwapongeza wananchi wa Botswana kwa hali ya utulivu waliyonayo na hivyo kuwa na amani na usalama katika maeneo yote.
Naye Balozi wa Ufaransa nchini Botswana amepongeza hali ya amani na utulivu iliyoko nchini Botswana wakati huu wakielekea katika uchaguzi mkuu na kuongeza kuwa ni jambo la msingi na la mfano kwa nchi za Afrika na nyinginezo.
Balozi wa Tanzania nchini Botswana mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini Mhe. James Bwana amepongeza kitendo cha Serikali ya Botswana kuruhusu na kuwakaribisha waangalizi wa uchaguzi nchini humo na kuwa tayari kushirikiana nao na kupongeza wananchi wa Botswana kwa utulivu waliounesha katika kipindi hiki na kuwatakia kila la heri katika uchaguzi mkuu ujao.
SEOM pia imekutana na viongozi wa vyama vya siasa vya BPF, BMD na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Botswana.
Katika mikutano na viongozi wa Vyama vya siasa viongozi wa vyama vya upinzani wameelezea kutokuridhishwa kwao na mwenendo wa uchaguzi huo wakisema kumekuwa na uhaba wa karatasi za kupigia kura hali ambayo inawatia wasiwasi juu ya uchaguzi huo kufanyika kwa uhuru na kwa haki na kuongeza kuwa kitendo cha kuchelewa kutangazwa kwa tarehe ya uchaguzi kumevifanya vyama vya upinzani nchini humo kutokuwa na maandalizi mazuri ya uchaguzi huo.
Chama cha BPF kimesema wanaamini kuwa kufanyika kwa kura za awali zilizohussisha Diaspora, vyombo vya ulinzi na usalama na majimbo matatu zitaongeza matumaini kwa wananchi na hivyo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo.
Nao MISA Botswana wamesema taasisi yao imekuwa ikijishughulisha na utoaji wa elimu kwa waandishi wa habari juu ya kuandaa na kuripoti taarifa za uchaguzi ila wanaelewa kuwa wanachama wao wanakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa taarifa zinazotolewa na wananchi kupitia mitandao ya kijamii ambao hawazingatii misingi na maadili ya uandishi wa habari