GABORONE-Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Kabo Morwaeng na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana, Mhe. Dkt. Lemongang Kwape alipotembelea Ofisi ya Rais wa Botswana jijini Gaborone.Mhe. Pinda amekutana na viongozi hao kwa lengo la kujitambulisha kama Mkuu wa Misheni ya SADC na kuwatambulisha wajumbe wa misheni hiyo ambao wako nchini Botswana kwa ajili ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Mhe.Pinda aliambatana na Sekretarieti ya SADC, wajumbe wa SADC Organ TROIKA, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, na Waangalizi wa SADC.
Mhe. Pinda aliwaambia wenyeji wake kwamba SEOM ipo Botswana tayari kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Mhe. Pinda aliisifu Botswana kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi pamoja na amani na usalama vilivyopo nchini humo, ambavyo vinaifanya Botswana kuwa bora zaidi.
Pia aliwapongeza kwa kuwa wazalishaji wakubwa wa madini ya almasi na kusaidia watu kutumia madini hayo halisi badala ya almasi bandia.
Kadhalika, aliwaambia wafikirie kuanzisha uzalishaji wa asali na bidhaa zake, kwani wana misitu katika nchi yao ambayo wanaweza kuitumia kama biashara kwa wakulima wao ili wapate kipato.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mhe. Kabo Morwaeng, aliikaribisha SEOM nchini Botswana na kumhakikishia kwamba Serikali ya Botswana iko tayari kufanya kazi nao na imejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu.
“Karibuni Botswana, hii ni nchi ya amani, na tumejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu unakuwa huru na wa haki kwa kila anayeshiriki,” alisisitiza.
Alisema, Serikali ya Botswana imejiandaa kwa uchaguzi mkuu na kwamba wako tayari kwa uchaguzi na kuihakikishia SEOM kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki na kuendelea kudumisha amani na usalama katika nchi yao.